na Abdallah Khamis
TUME ya
Uchaguzi nchini (NEC) inadaiwa kuingia katika mchakato wa mwisho wa
kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za
M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution zinazodaiwa kuwa na
rekodi mbaya ya utendaji.
Tanzania
Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unahusishwa na njama za kutaka
kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo kwa kuchakachua
matokeo ya kukibakiza madarakani.
Kampuni
hizo ambazo katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zimetajwa kushirikiana na
Kampuni ya Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited, mbali ya kutojulikana
zinapotoka, pia ndizo zimekuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine
zilizoomba kazi hiyo.
Kiwango
ambacho kampuni hizo zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa
vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric Voters
Registration) ni zaidi ya euro milioni 60, sawa na sh bilioni 126.3,
wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia euro milioni 40.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe,
ni mmoja wa viongozi waliofichua mkakati huo, akidai unafanywa na
serikali ya CCM ili kuhakikisha wanajiandaa kudhibiti kila eneo ili
waweze kubaki madarakani.
Alisema
lengo ni kuhakikisha mchakato wa vitambulisho vya kupigia kura vya
kielektroniki vina kuwa na faida kwa CCM na kukiingizia fedha chama
hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo kupitia mfumo huo dhaifu wa
vitambulisho hivyo.
Zitto
alisema kutokana na hali hiyo, amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Serikali (CAG) barua ya kutaka ukaguzi wa zabuni hiyo ufanyike kwa
kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na
vyombo vingine vya usalama kwa ajili ya kujiridhisha.
"Wenzetu
CCM wanafanya mikakati ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa
kuhakikisha wanapata fedha za kutosha na hata mazingira mabaya ya vifaa
vitakavyotumika katika upigaji kura na sasa wameshaingia hata katika
Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza mazingira," alisema Zitto.
Aliongeza
kuwa kiasi kilichotolewa ni kodi ya Watanzania na kwamba ni vema taifa
likajiridhisha kuwa matatizo yaliyotokea Kenya na Ghana hayatajirudia
Tanzania, hasa wakati wa upigaji kura.
Gazeti
hili limeona barua hiyo ya Zitto kwenda kwa CAG, ya Novemba 7, 2013,
yenye kichwa cha habari; 'Zabuni ya Biometric Voters Registration (BRV
KITS) No. IE/018/2012-13/HQ/G/19 yenye thamani ya sh bilioni 126.3.'
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu.
"Zabuni
hiyo sasa imeanza kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kutokana na
kinachosemekana kuwa kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina uwezo
kiteknolojia, pia bei zao ni kubwa.
"Katika
mafunzo ya hivi karibuni ya SADCOPAC jijini Nairobi tuliazimia kuwa ni
vema kwenye zabuni nyeti kama za namna hii, SAIs wawe na uwezo wa
kufanya ukaguzi kabla ya zabuni kutolewa na kuanza kutekelezwa,"
alisema.
Kwa
mujibu wa nyaraka za NEC ambazo Tanzania Daima linazo, kampuni
zilizopewa tenda ya pamoja yenye kugharimu kiasi cha dola 78,
987,636.00, sawa na sh 126,291,375,455 ni M/S Jazzmatrix Cooperation na
M/S Invu IT Solution ambazo hazijulikani nchi zinapotoka zikiwa
zinashirikiana na M/S SCI Tanzania Limited.
Katika
nyaraka hizo kampuni zilizokosa tenda na ambazo zimelalamika kwa
Mkurugenzi wa NEC namna mchakato wa kutoa zabuni hiyo ulivyoendeshwa
zimeainishwa kuwa ni M/S Zetes SA ya nchini Ubalgiji, M/S IRIS
Corporation Technology ya Malaysia, M/S Lithotech Exports ya Afrika
Kusini, M/S Safran Morpho ya Ufaransa na M/S Avante International
Technology, Inc ya Marerkani.
Kampuni
hizo zinahoji njia na sababu zilizowafanya wakose tenda hiyo licha ya
kuwa na uzoefu, vifaa bora pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha gharama
tofauti na kampuni iliyopewa kazi.
Katika
moja ya malalamiko yao, Kampuni ya M/S Morpho, inalalamika
kutofahamishwa namna walivyokosa vigezo vya kupata kazi hiyo licha ya
kuwa na sifa za kimataifa za kufanya kazi huku ikiwa imetoa bei nafuu
kuliko kampuni iliyopata kazi.
"Tulikuwa
miongoni mwa washindani muhimu kwa kuwa kiwango chetu kilikuwa ni sh
bilioni 97.8 ambazo ni sawa na euro 44,939,912 + sh 3,843,736,140.
"Ujuzi,
vigezo na uzoefu wetu havilingani, duniani kote tumefanya kazi katika
maeneo mengine kwa ufanisi na tunashindwa kuelewa kivipi walishinda hao
ambao wamepata kazi kwa kiwango cha zaidi ya sh bilioni 27.8
ikilinganishwa na yetu," ilisomeka sehemu ya barua.
Alipotafutwa
Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema hawezi kuliongelea suala
hilo katika simu na kuomba mwandishi awasiliane na Kaimu Mkurugenzi wa
NEC, Dk. Sist Cariah, ambaye alisema mchakato wa kupata kampuni
ulifuatwa kisheria.
Dk.
Cariah alisema si kweli kwamba kampuni iliyopewa kazi haina uwezo bali
malalamiko yanatoka kwa watu walioshindwa kupata kazi hiyo.
Alipoulizwa
juu ya uzoefu wa kampuni hiyo na wapi ilifanya kazi, Dk. Cariah alisema
kwa maelezo waliyonayo ni kwamba kampuni hiyo ina uzoefu wa miaka 35 wa
kufanya kazi, huku akishindwa kuainisha sehemu ilizowahi kufanya kazi.
Kuhusu
wapi zimetoka kampuni hizo, Dk. Cariah alisema suala la kutoainishwa
kimaandishi ni makosa ya kawaida, huku akitaja kuwa zinatoka katika nchi
ya India na Australia.
Kuhusu
gharama, Dk. Cariah alisema licha ya makampuni mengine kutaja gharama za
chini, zingeweza kuwa na gharama kubwa zaidi wakati wa kukamilisha kazi
hiyo kutokana na kuwa na gharama zilizojificha.(CHANZO TANZANIA DAIMA)
No comments:
Post a Comment