Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, December 4, 2013

JK:TUTAONDOA CHANGAMOTO ZA WENYE ULEMAVU NCHINI


mwinyi  Waziriwa Afya na Ustawi wa jamii Dk Hussein Mwinyi akizungumza jana katika uzinduzi wa mpango wa wadau wa ushirikiano wa kuthibiti sumu kuvu(Aflatoxins) ipatikanayo katika vyakula vya mazao na mifugo barani Afrika .Picha na Aika Kimaro 
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inaondoa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini ili kuwawezesha kushiriki vyema katika shughuli za maendeleo.
Akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani jana jijini Dar es Salaam, Kikwete alisema kwa kuanzia Serikali itahakikisha wananchi hao wanatafutiwa mkalimani kwenye Televisheni ya Umma, kuwekewa miundombinu rafiki katika majengo pamoja na kupewa ruzuku za vyama vyao kwa wakati.
“Ruzuku inayotolewa kwenye vyama vya watu wenye ulemavu haitoshi na hakuna siku zitatosha,lakini tutaendelea kuongeza. Naomba kanuni za matumizi ya fedha yazingatiwe msipate shida wakati wakaguzi wanapokuja kukagua mahesabu,”alisema.
Alisema pamoja na mipango ya Serikali,siku hiyo itumike katika kuikumbusha jamii juu ya umuhimu na ustawi wa watu hao wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutambua mafanikio na changamoto wanazokutana nazo katika maisha yao ya kila siku.
“Ulemavu siyo kizuizi cha kumfanya mtu ashindwe kushiriki kwenye ujenzi wa taifa…, asilimia kumi ya Watanzania ni walemavu, ni wanadamu kama walivyo watu wengine hata mahitaji yao ni sawa,” alisema Kikwete.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dk Hussein Mwinyi alisema, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuvifanyia ukarabati vyuo vya watu wenye ulemavu nchini na kutoa rai kwa wananchi kuhakikisha watu wenye sifa wanajitokeza.
“Serikali inaendelea kuondoa vizuizi vinavyowakabili kwa kutoa vifaa na mashine wanavyohitaji,” alisema.
Akisoma risala kwa niaba ya Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shuvyawata) na wadau,Amon Anastazi aliiomba Serikali kuhakikisha kuwa vyombo vyote vya usafiri vinavyoingia nchini vinakuwa na vigezo vya kimataifa vinavyowawezesha watu wenye ulemavu kupanda na kuteremka bila tatizo.
Pia Anastazi aliiomba Serikali kuhamisha idara inayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kupelekwa Ofisi ya Rais kwa madai kuwa ofisi hiyo ina uwezo zaidi wa kutatua matatizo yao.
“Tunataka idara hii ihamishiwe sehemu ambayo ina mamlaka ya kuziamuru wizara zingine zinazohusika na walemavu kuwajibika,kwa mfano kule Zanzibar idara hiyo imewekwa kwenye Ofisi ya Makama wa Rais,”alisema.
Katika maadhimisho hayo rais pia aliwatunuku vyeti wadau mbalimbali waliotoa mchango mkubwa kwa walemavu ikiwa ni pamoja na kuzindua alama maalumu za barabarani kwa ajili ya walemavu.

No comments:

Post a Comment