WAFANYAKAZI wawili wa Kampuni ya Uwakala
wa Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO),
wanashikiliwa Polisi kwa madai ya kupanga njama za kupitisha
wasafirishaji wa dawa za kulevya katika uwanja huo.
Jana Polisi mkoani Kilimanjaro ilikamata
wafanyakazi hao (majina tunayo), kwa tuhuma za kusafirisha hadi
uwanjani hapo wanawake wawili raia wa nje, wanaodaiwa kukamatwa na dawa
za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 15 mwishoni mwa wiki.
Taarifa kutoka katika uwanja huo,
zilidai kuwa wafanyakazi hao, ndio waliohusika kusafirisha watuhumiwa
hao raia wa Nigeria na Liberia mpaka katika uwanja huo na walifika saa 9
mchana Jumamosi iliyopita.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari
kutoka uwanjani hapo, wanawake hao wawili walitumia gari aina ya Noah,
linalodaiwa kumilikiwa na mmoja wa wafanyakazi hao.
Mtoa habari wetu alidai kuwa baada ya
kufikisha wageni hao uwanjani, mwanamke Mnigeria aliyekuwa na kilo 10 za
dawa hizo, aliandaliwa mazingira ya kupita uwanjani hapo bila
kukaguliwa, lakini kwa bahati mbaya alikuwa ameshachelewa ndege.
Kutokana na hali hiyo, aliandaliwa
usafiri mwingine wa Shirika la Ndege la Precision kwenda Nairobi kuanzia
saa 11 alfajiri ya juzi. Mwenzake Mliberia anayedaiwa kuwa na kilo tano
za dawa hizo, aliandaliwa usafiri wa Shirika la Ndege la Ethiopia na
alitarajiwa kuondoka uwanjani hapo saa tisa usiku wa kuamkia juzi pia.
Taarifa hizo zilidai kuwa wafanyakazi
hao kwa kuwa hawakuwa zamu usiku, walikabidhi wageni hao kwa mfanyakazi
mwenzao na kumlipa ili asaidie wapite uwanjani hapo bila kukamatwa.
Hata hivyo, inadaiwa mfanyakazi huyo
muda ulipofika, aliondoka eneo la kazi na kuaga kwenda kunywa chai na
kumwacha mwingine, hatua iliyosababisha wakamatwe.
Juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Boaz, alithibitisha kukamatwa kwa raia hao wa kigeni
na akaahidi angewataja majina jana, lakini hakufanya hivyo.
Gazeti hili lilipomtafuta jana, kupata
majina ya watuhumiwa hao na kuthibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa
wengine, simu yake ilipokewa na msaidizi wake, ambaye alisema Kamanda
Boaz alikuwa katika kikao cha ndani asingeweza kuzungumza.CHANZO HABARI LEO
No comments:
Post a Comment