NAIBU
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHE. LAZARO NYALANDU (KUSHOTO)
AKIZUNGUMZA NA WANAHABARI (HAWAPO PICHANI) ALIPOKUWA AKIZUNGUMZIA
MSIMAMO WA SERIKALI JUU YA MATUKIO YA UJANGILI NCHINI. KULIA NI KAIMU
MKURUGENZI WA IDARA YA WANYAMAPORI PROFESA JAPHARY KIDEGHESHO.
Tembo 60 wameuawa na majangili kwenye hifadhi mbalimbali nchini katika mwezi mmoja tangu operesheni tokomeza isitishwe.
Mauaji hayo yametajwa kufanyika katika Hifadhi za Selous, Rungwa, Burigi, Katavi na Ngorongoro.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema jana kwamba
idadi hiyo ni sawa na wastani wa tembo wawili kila siku, inakwenda
sanjari na kuuawa, kujeruhiwa kwa watumishi kadhaa wanaofanya kazi
kwenye hifadhi.
Alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu namna serikali ilivyojipanga kuhakikisha inatokomeza vitendo vya
ujangili.
Alitaja askari wa wanyamapori, Ramadhani Magengere (40) aliuawa na
majangili na wakati huo huo, Yahya Ramadhani (34) alijeruhiwa na
wafugaji walioingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jumuiya
(WMA) Ukutu iliyoko Morogoro Vijijini.
Matukio hayo ni ya Desemba 6 mwaka huu.Aidha alisema Novemba 14,
mtumishi wa wanyamapori, Sajid Majidi alijeruhiwa kwa kuchomwa mkuki
kichwani na kuvunjwa mkono na wafugaji walioingiza ng’ombe katika eneo
la Ramsar, Kilombero.
Alisema wapo watumishi wa pori la akiba Mkungunero wilayani Kondoa,
Dodoma, waliokuwa doria walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 80
waliokuwa na mikuki na silaha nyingine za jadi na kujeruhiwa.
“Kutokana na kusitishwa kwa operesheni tokomeza, matukio ya uvunjaji wa
sheria za hifadhi kama vile uingizaji holela wa mifugo katika maeneo ya
hifadhi, ujangili wa wanyama wakiwemo tembo pamoja na uvunaji wa miti
katika hifadhi za misitu, bado yanaendelea,” alisema.
Aliendelea kusema, “Majangili wameua tembo 60 katika hifadhi na mapori
ya Selous, Rungwa, Burigi, Katavi na Ngorongoro….. hawa ni takribani
tembo wawili kwa siku na ikumbukwe wakati wote wa operesheni tokomeza
iliyodumu mwezi mmoja ni tembo wawili tu waliokuwa wameuawa,” alisema
Nyalandu.
Naibu Waziri alisema serikali imegundua kambi ya majangili iliyoanzishwa
katika pori la akiba la Burigi ambako vitendo vya ujangili vinaendeshwa
na baada ya kukurupushwa na askari wa wanyamapori walikimbia na kuacha
nyama ya nyani 30 waliokuwa wamewaua.
Aidha alisema hivi karibuni, wilayani Simanjiro, lilikamatwa gari likiwa
limejaa mizoga 20 ya swala. Alisema lipo ongezeko la wimbi la uvamizi
na ufugaji wa mifugo ndani ya mapori ya akiba, hifadhi za misitu iliyoko
Magharibi mwa nchi hususani Burigi, Biharamulo, Kimisi, Moyowosi,
Katavi na Ugalla.
“Serikali inawakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa sheria ya
wanyamapori namba 5 mwaka 2009 pamoja na sheria zinazosimamia maeneo ya
hifadhi za taifa na misitu kuwa hawaruhusiwi kuingiza mifugo wala
kuingia kuua, kuwinda, kukamata wanyama bila kibali cha mkurugenzi wa
wanyamapori,” alisisitiza.
Wakati operesheni tokomeza imegeuka kuwa mwiba baada ya wabunge kuibua
kashfa ya unyanyasaji na utesaji uliofanywa na wananchi hivyo
kusababisha mawaziri kadhaa kujiuzulu, Nyalandu alisema matukio hayo
ya bungeni Dodoma, hayajatengua sheria yoyote ya Wanyamapori au Misitu.
Aliwaagiza watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yao
ya ulinzi wa maeneo ya hifadhi za taifa, mapori ya akiba na misitu ya
hifadhi bila kutetereka.
Alitaka wachukue hatua stahiki dhidi ya mhalifu yeyote ilimradi
wanazingatia sheria. “Ikumbukwe kuwa matukio yaliyotokea bungeni Dodoma,
hayajatengua sheria yoyote… hamna maamuzi yoyote ya Bunge
yaliyohalalisha ukiukwaji wa Sheria za Uhifadhi,” alisema Nyalandu.
Alisisitiza kwamba wananchi wanatakiwa kutii na kufuata sheria hizo kama
zilivyo. “Tahadhari inatolewa kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua
kali yeyote atakayekiuka Sheria ya Wanyamapori kwa makusudi.
Tunawaomba wananchi wasikubali kudanganywa na mtu yeyote kuvunja sheria
za nchi,” alisema. “Serikali inasisitiza kuwa kwa kutumia vyombo vyake
itaendelea kutimiza majukumu yake ya kusimamia ipasavyo sheria, ikiwa
ni pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayeshiriki moja kwa
moja au kusaidia vitendo vya ujangili ili kunusuru rasilimali za
taifa,” alisisitiza.
Katika mkutano huo wa jana, Naibu Waziri asisitiza serikali ina maadili
na miiko ya utendaji kazi kwa watumishi wake wakiwemo askari wa
wanyamapori. Alisema serikali itaendelea kuwakumbusha watumishi maadili
na miiko kila wakati kupitia mafunzo na mbinu nyingine.
Operesheni Tokomeza ilisitishwa Novemba mosi kabla ya wabunge kuibua
kashfa ya unyanyasaji na utesaji unaodaiwa kufanywa na waliokuwa
wakiiendesha na hivyo kusababisha mawaziri wanne kuachia nyadhifa zao.
Ripoti ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
iliyoundwa kuchunguza operesheni hiyo, ilieleza kuwa athari zilizotokana
na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne zilizokuwa zikiongozwa
na mawaziri hao.
Mawaziri walioachia nyadhifa zao ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki aliyejiuzulu na wengine wanne ambao kwa pamoja,
Rais Jakaya Kikwete alitengua nafasi zao.
Wengine ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi, Dk Mathayo David, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha.
No comments:
Post a Comment