Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA
Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amekubali kushuka cheo
hadi kuwa Kocha Msaidizi wa klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam na wakati
wowote atasaini Mkataba wa kuanza kazi Jangwani.
Mkwasa
aliiongoza kwa mara ya mwisho Ruvu Shooting jana ikifungwa mabao 3-0 na
Azam FC katika mchezo wa kirafiki, Uwanja wa Azam Complex na baada ya
mechi hiyo akasema; “Kweli, niko njiani kurejea Yanga, lakini bado
sijasaini Mkataba, tumefikia makubaliano tu,”alisema kiungo huyo wa
zamani wa kimataifa wa Tanzania.
Mkwasa
amesema makocha wengi wa Tanzania kwa sasa wanaogopa kufanya kazi timu
za Simba na Yanga kutokana na desturi ya kufukuza walimu ovyo, lakini
yeye anajiamini atafanya kazi nzuri ambayo itamuepushia ‘balaa’ la
kutupiwa virago.
“Mimi
ni mwalimu ambaye najiamini, naweza kufanya kazi sehemu yoyote wakati
wowote, hii Yanga SC mimi nimekwishafanya kazi kwa mafanikio kama
mchezaji na kama kocha pia, sina wasiwasi wowote,”alisema Mkwasa maarufu
kama Master enzi zake anatamba katika safu ya kiungo.
Charles
Boniface Mkwasa aliyezaliwa Aprili 10, mwaka 1955 mjini Morogoro
alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza kama mchezaji mwaka 1978
akitokea Tumbaku ya Morogoro na akacheza hadi 1988 alipostaafu na kwenda
kuanza maisha ya ukocha katika klabu ya Super Star ya Dar es Salaam
mwaka 1989.
Mwaka
1990 kwa ufadhili wa waliokuwa wafadhili wa Yanga SC, chini ya marehemu
Mohamed Viran ‘Babu’, Mkwasa alikwenda kusomea ukocha nchini Brazil na
aliporejea akawa kocha Msaidizi wa Yanga chini ya marehemu Syllersaid
Salmin Kahema Mziray.
Mkwasa
alianza vizuri Yanga SC baada ya kuiwezesha kufika Fainali ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati visiwani Zanzibar mwaka 1992 ambako
walifungwa na Simba SC kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya
dakika 120.
Mwaka
1993 Mkwasa akiwa Msaidizi wa Mrundi, marehemu Nzoyisaba Tauzany
‘Bundes’ akaiwezesha Yanga kutwaa Kombe hilo ambalo sasa linaitwa Kagame
mjini Kampala, Uganda kabla ya mwaka 1994 kuhamia Sigara alipokwenda
kuwa Kocha Mkuu.
Mkwasa
aliifanya Sigara kuwa tishio katika soka ya Tanzania hadi kushiriki
michuano ya Afrika, kabla ya kutupwa na kampuni na timu kuchukuliwa
wafanyabiashara kuanzia Azim Dewji, baadaye Alex Kajumulo na Merey
Balhaboub. TCC ilipoitema Sigara, Mkwasa akaenda kufundisha nje ya nchi
kwa mara ya kwanza, katika klabu ya Al Khaboura ya Oman mwaka 1997.
Alikaa
Oman kwa msimu mmoja kabla ya kurejea mwaka 1998 na kujiunga na Prisons
ya Mbeya, ambayo mwaka 1999 aliipa ubingwa wa iliyokuwa Ligi Kuu ya
Muungano na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2000.
Mume
huyo wa Betty Mkwasa mwaka 2000 alikwenda Ujerumani kusomea ukocha na
aliporejea mwaka 2001 akajiunga na Coastal Union ya Tanga kabla ya mwaka
huo huo baadaye kuajiriwa tena na Yanga kama kocha Mkuu, akichukua
nafasi ya Mkongo Raoul Jean Pierre Shungu.
Master
Mkwasa aliendelea kuwa kocha wa mafanikio Jangwani baada ya kuiwezesha
timu hiyo kufika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa, ambako ilitolewa
kwa mbinde na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 6-5,
sare ya 3-3 Mwanza na kufungwa 3-2 Afrika Kusini.
Mwaka
2003 Mkwasa aliachana na Yanga akaenda kufungua kituo chake cha mafunzo
ya soka kwa vijana, Pangolin kilichoibua vipaji kadhaa kabla ya mwaka
2005 kuchukuliwa na Moro United, enzi hizo ikiwa chini ya bilionea Merey
Balhaboub.
Mkwasa
aliifanya Moro kuwa tishio na hadi ikacheza Fainali ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati mwaka 2006 mjini Dar es Salaam ikifungwa 2-1 na
Polisi ya Uganda iliyoibuka bingwa, katika mechi pekee ya klabu
kuhudhuriwa na Rais wa sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Mrisho Kikwete.
Mwaka
2007 Mkwasa akaenda Miembeni ya Zanzibar aliyoipa ubingwa wa visiwani
humo kabla ya 2009 kuja Dar es Salaam kuifundisha African Lyon hadi 2010
alipokwenda Ruvu Shooting ya Pwani, ambako amefanya kazi hadi sasa
anarejea Yanga kama kocha Msaidizi.
Mkwasa
pia amefundisha kwa mafanikio timu za taifa kuanzia za vijana, wakubwa
hadi wanawake, mwaka 2001 akiwa na marehemu Mziray waliipa Taifa Stars
Kombe la Castle mjini Mwanza wakati timu ya wanawake, Twiga Stars ameipa
tiketi mbili za michuano ya Afrika, Mataifa ya Afrika 2010 na Michezo
ya Afrika 2012.
Yanga
inamchukua Mkwasa kuwa Msaidizi wa kocha mpya wanayemtafuta kwa sasa,
baada ya kufukuza benchi zima la Ufundi chini ya Kocha Mholanzi, Ernie
Bradts na Wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Razack Ssiwa.
No comments:
Post a Comment