JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
MKOA WA RUKWA
Telegraphic: “REGCOM”
Simu. No:0252802137/2802138/2802144
Fax No. (025) 2802217/2802318
E-mail:rasrukwa@yahoo.com
|
OFISI YA MKUU WA
MKOA,
P. O.
Box 128,
SUMBAWANGA.
|
TAARIFA KWA UMMA.
Serikali
Mkoani Rukwa inapenda kukanusha taarifa iliyotolewa na gazeti la Jambo Leo
toleo namba 1546 la tarehe 3, Disemba 2013 iliyoandikwa na Mwandishi Gurian
Adolf katika ukurasa wa 10 iliyokuwa na kichwa cha habari "TCCIA Rukwa
yaomba mbolea ya DAP".
Sehemu
ya taarifa hiyo ilieleza kuwa; Nanukuu "Mwenyekiti wa Chama cha
Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Rukwa, Shadrack Malila
ameiomba Serikali kuwashauri wakulima wa Mkoa huo kutumia mbolea nyingine ya
kupandia mahindi badala ya mbolea ya minjingu ambayo haijafanyiwa utafiti
katika Mkoa huo."
Kwa
mujibu wa gazeti hilo taarifa hiyo aliitoa mbele ya waandishi wa habari Ofisini
kwake mjini Sumbawanga ambapo aliongeza kuwa "Tangu awali wakulima hao
walikataa mbolea hiyo, baada ya kuitumia kupandia na kushindwa kustawisha
vizuri mazao yao ya mahindi, tofauti na mbolea ya DAP ambayo husaidia
kupatikana kwa mazao mengi”. Mwisho wa kunukuu.
Serikali
Mkoani Rukwa inapenda kukanusha kuwa sio kweli kwamba mbolea ya minjingu
haijafanyiwa utafiti kufaa kutumika katika Mkoa huu na kwamba haijapokea
malalamiko yeyote yaliyo rasmi kutoka kwa wananchi (wakulima) juu ya ubora na
ufanisi wa mbolea hiyo. Matokeo yake yameonekana kuwa ni mazuri hususani baada
ya mbolea hiyo kuboreshwa zaidi na sasa inaitwa "Minjingu Mazao".
Napenda
ifahamike wazi kuwa tafiti mbalimbali za udongo zimefanyika Mkoani Rukwa mfano, taarifa ya BRALUP, 1977, Tafiti za udongo zilizofanywa
na Kituo cha Utafiti cha Uyole na Sampuli mbalimbali zilizopelekwa Chuo Kikuu
cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nkasi miaka ya
2008-2010 na kuonesha sehemu kubwa ya udongo wa maeneo ya Uwanda wa juu wa
Ufipa (Ufipa Plateau) kuna upungufu
mkubwa wa kirutubisho cha aina ya Naitrojeni kulingana na mahitaji yake kwa
mimea jamii ya nafaka, hasa mahindi chotara.
Aidha,
majaribio ya kutumia aina na viwango mbalimbali vya mbolea kwa zao la mahindi
ikiwemo Minjingu yamefanywa kupitia Kituo Kidogo cha Utafiti cha Uyole
kilichokuwa wataalam huko Nkundi na mashamba ya majaribio sehemu mbalimbali na
kutoa matokeo yaliyofanyiwakazi. Kufuatia majaribio hayo, Mkoa wa Rukwa ulitoa
mapendekezo kwa kampuni ya Minjingu Mines & Fertilizer ya kubadilishwa kwa
umbile la mbolea ya Minjingu kutoka katika umbile la unga (powder form) na kuwa katika umbile la sasa la chengachenga ili
kuwa rahisi wakati wa kuweka mbolea shambani. Pia Mkoa ulipendekeza mbolea hiyo
iwekewe kirutubisho aina ya Nitrojeni ili kukidhi mahitaji ya udongo wa sehemu
kubwa ya Ukanda wa juu wa Ufipa, mapendekezo ambayo yamezingatiwa zimefanywa na
matokeo yake kuonekanika.
Mashamba
Darasa yanayohusisha mbolea ya Minjingu Mazao yameanzishwa na kuendeshwa sehemu
mbalimbali za Mkoa katika msimu uliopita wa 2012/2013 na kukaguliwa na Viongozi
kuona ufanisi wake. Yapo mashamba yaliyofanya vizuri na yapo ambayo hayakufanya
vizuri. Hali ya tofauti kama hiyo hutokea kwa aina zote za mbolea zinapotumika
katika maeneo tofauti. Ikumbukwe kuwa ardhi ipo hai na hutofautiana
kutoka sehemu moja na nyingine!
Tafiti
nyingi zimeonesha kuwa wakulima wengi wameshindwa kupata matokeo mazuri katika
kilimo kwa kushindwa kufuata masharti ya wataalam wa kilimo hata kama wakitumia
mbolea ya aina yeyote. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa Kauzeni na
wenzake katika vijiji vya Ntendo na Mtimbwa mwaka 1998, pamoja na mambo mengine
ilibainika kuwa wakulima wachache waliomudu kutumia mbolea au mbegu bora
hawakuzingatia viwango vilivyopendekezwa na wataalam. Walitumia karibu nusu tu
ya mapendekezo, Mfano Hekta moja iliyopandwa mahindi zilitakiwa kutumia kilo
125 za TSP Triple Super Phosphate ( P2O5
) 18% na kilo 250
za UREA (N) 46%, ili kuvuna tani sita za mahindi sawa na kilo 6,000 au wastani
wa magunia 60 kwa hekta. Waliofanya vizuri kidogo walitumia kilo 100 tu za TSP
na kilo 100 za UREA.
Kufuatia
taarifa hiyo, Uongozi wa Mkoa wa Rukwa haupendi kuingilia uhuru wa mtu wa
kupata na kutoa habari kama Mtanzania mwingine yeyote. Ni vema mtu akatoa taarifa anazozifahamu vizuri/zilizofanyiwa
utafiti, zisizoleta mtafaruku au kuipotosha jamii na zisizolenga kuvutia
maslahi binafsi kwa namna yeyote ile.
Serikali
ya Mkoa imesikitishwa na taarifa aliyoitoa Bwana Malila. Ni dhahiri kuwa
ametumia vibaya nafasi yake ya uenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Rukwa kuwashawishi
wakulima wa Mkoa huu kuwa mbolea ya Minjingu haifai na haitowapa mavuno mazuri.
Ikumbukwe kuwa Bwana Malila ambae ni msambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya
Serikali katika Manispaa ya Sumbawanga kwa mwaka huu 2013/14 pia ni
mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea anayoipigia chapuo ya Diammonium
Phosphate maarufu kama DAP.
Ifahamike
pia kuwa Bwana Malila aliwahi kuwa na Mkataba na Kampuni ya Minjungu Mines
& Fertilizer Ltd katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/2010. Kama kweli
mbolea hiyo haifai mbona aliwahi kuwa wakala na akaisambaza kwa wakulima bila
kutoa matamko kama haya? Ni dhahiri kuwa taarifa yake hiyo ina mgongano wa
kimaslahi na hailengi katika kuboresha kilimo kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa.
Imetolewa na:
Albinus Mugonya,
Kaimu
Katibu Tawala Mkoa,
RUKWA.
10
Disemba, 2013
No comments:
Post a Comment