TUNAJUA shangazi anatutesa kwa sababu baba na mama wapo mbali, kama wangekuwepo hapa tusingeteswa hivi.
Tunamuomba baba, tunamuomba
mama kama watasoma habari hii waje watuchukue turudi nyumbani, shangazi
anatutesa sana, wala hatukutegemea,” ndivyo alivyoanza kusema mtoto
Hassan Yusuf (5) ambaye ni mkubwa kwa wenzake, Hussein Yusuf (5) na
Rehema Said (5).
Ikifika mahali mtoto mdogo
anasema anawakumbuka wazazi wake kwa sababu ya mateso anayoyapata
ugenini ujue ni zaidi ya ukatili, tena ni ukatili wa kutisha.
Watoto hao, kwa sasa wanaishi
Nzasa ‘A’, Kata ya Charambe, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na
ndiko walikopatia mateso yote.MAMBO YALIPOANZA KUTIBUKA
Wiki iliyopita, watoto hao
waliokolewa na majirani katika kifungo cha miezi sita ndani huku afya
zao zikiwa zimedhoofu kwa kukosa chakula.
Ilidaiwa kwamba, watoto hao
Hassan na Hussein ambao ni mapacha na Rehema, walifungiwa katika banda
la shangazi yao aitwaye Asia Bora ambalo ujenzi wake haujakamilika.
Wamekuwa wakiishi humo kwa kula mabaki ya vyakula jalalani.
Watoto Hassan Yusuf, Hussein Yusuf na Rehema Said baada ya kuokolewa na majirani.
USHUHUDA WA MAJIRANI
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni, majirani wa nyumba hiyo
walimweleza mwandishi wetu kuwa watoto hao wamekuwa wakionekana nje ya
nyumba hiyo mara chache sana wakiwa wanagombania mabaki ya vyakula
kwenye jalala.
“Tumekuwa tukiwaona nje mara chache kwenye jalala. Unajua, Asia
(shangazi yao) aliwachukua kwa kaka yake, Kijiji cha Namakongoro Kata ya
Lihimalyao huko Kilwa mkoani Lindi.
“Tukasikia lengo lake aje kuishi nao kwa vile yeye Mungu hamkujalia
kupata watoto. Lakini maisha hapo kwake yakawa siyo mazuri kwa kipato
kwa mama huyo.
Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Ramadhan yeye alikwenda mbele zaidi kwa kusema:
“Hapo awali tulikuwa tukiwaona wakitoka nje na kucheza na watoto wetu
huku wakiwa na afya nzuri. Asia akatueleza kuwa ni watoto wa nduguye,
amewachukua huko kijijini.
“Baada ya muda fulani tukawa hatuwaoni, tulidhani amawarudisha kwao,
lakini kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda mbele tukawa tunawaona mara
chache wakiwa jalalani wanapigania mabaki ya chakula.
“Kuna siku mimi niliwakamata wakiwa wamebeba mfuko wa rambo wenye
kinyesi, walikuwa wanakuja kutupa katika maeneo yetu, nikawarudisha nao
kwa shangazi yao. Kumbe nyumba wanayoishi haina choo ndiyo maana
wamekuwa wakijisaidia kwenye rambo.
“Siku moja walipotoka nje kutafuta chakula jalalani, mimi na majirani
wenzangu tuliwauliza wanaishije? Wakatuambia hawapewi chakula na
shangazi yao akitoka asubuhi harudi mapema, akirudi inakuwa ni usiku
sana wao wakiwa wameshalala.
“Inasikitisha sana kuwaona watoto hawa wanaachwa peke yao kutwa nzima
bila mtu wa kukaa nao na wamekuwa wakifungiwa ndani kwa muda mrefu
sasa, ila huwa wanakiuka masharti na kutoka kwa ajili ya kutafuta mabaki
ya chakula.
Jirani huyo akaendelea kuanika mateso ya watoto hao: “Kwa kuwaonea
huruma tumekuwa tukilazimika kuwapa chakula, lakini Asia anaporudi na
kugundua hilo anawapiga, kwa hiyo wakawa waoga kuja kuchukua chakula.
Mimi niliumia hadi machozi.”
Jirani: “Baadaye wakawa hawaonekani, lakini cha ajabu mara nyingi
tukiamka asubuhi tunakuta mifuko ya rambo yenye vinyesi imetapakaa,
tukimweleza Asia inakuwa ugomvi.
“Siku moja baada ya shangazi yao kuondoka, nilikwenda kuwachungulia
ndani, nikawaona wamekonda sana, wamepauka na wamevaa nguo zilizochakaa.
“Nilitokwa machozi, nililazimika kuwaita wenzangu nao walipofika
hakuna aliyejizuia kulia. Tukasema hawa watoto watakufa, ndiyo tukaamua
kuwaokoa kwa kupeleka taarifa kwa mzee Dadi Salum ambaye ni polisi jamii
wa hapa.
POLISI JAMII NAYE ALIA
“Mzee Dadi naye alipofika na kuwaona kwa macho alilia, watu wakaanza
kukusanyika, tukawatoa nje watoto, kila mmoja aliwaonea huruma.
Tuliwachukua hadi Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Nzasa A.
SHANGAZI MTU ANUSURUKA KIPIGO
“Hatujui ni nani aliyempigia simu Asia, kwani muda mfupi tu tukasikia
yupo nyumbani kwake. Uongozi wa mtaa ulimfuata, walipofika, wanawake
wenzake hasa wale anaochukua nao mkopo wa fedha benki walitaka kumpiga
wakimuuliza pesa anapeleka wapi.
“Hata hivyo aliokolewa na polisi jamii ambao walimchukua na kumweka
katika Bajaj na kumpeleka Kituo cha Polisi Mbagala kwenye Dawati la
Jinsia na Watoto, watoto nao pia walipelekwa huko.”
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzasa A, Mrisho Salum alikiri
kuwapokea watoto hao wakiwa katika hali mbaya kiafya, wakapelekwa
polisi. Akawataka wananchi kutokaa kimya mara wanapoona vitendo kama
hivyo.
Mwandishi alifika hadi kituo cha polisi na kuambiwa na askari mmoja
kuwa mapacha walichukuliwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Othman
Mbwana aliyedai ni babu yao.
Mbwana alidai kwamba ameamua kuwachukua watoto hao wakaishi nyumbani kwake wakati akifanya mawasiliano na wazazi wao.
“Kwanza nitawapeleka hospitali wakatazamwe afya zao, ila
nimesikitishwa sana na hali hii, sijajua ni kwa nini watoto hawa
wamefikia hatua hii,” alisema Mbwana.
Rehema yeye alichukuliwa na mjomba wake aitwaye Sood Ismail ambaye
alidai anakwenda kukaa naye hadi hapo atakapofanya mawasiliano na wazazi
wa huyo mtoto, akisema kitendo cha Asia kimeidhalilisha familia.
RPC KIONDO
RPC TEMEKE ATUPIA NENO
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo amewataka wananchi kufichua
vitendo viovu ndani ya jamii na amewapongeza vijana wake wa ulinzi
shirikishi kuokoa maisha ya hao watoto.
No comments:
Post a Comment