…………………………………………………………………………
NA MWANDISHI WETU, Dodoma
WAKATI Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
imekamilisha kazi ya kuwahoji baadhi ya viongozi wa chama hicho
wanaotajwa kuanza mbio za kusaka urais 2015, kabla ya muda, zimeanza
kuvuja fununu za najama za kusukwa hujuma dhidi ya Katibu Mkuu wa chama
hicho, Abdulrahaman Kinana na Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula.
Hujuma hizo ni kutoka kwa moja ya makundi ya mitandao ya wasaka
urais, ambayo mgombea wao mtarajiwa ni kati ya waliohojiwa kwa muda
mrefu kuanza kampeni mapema.
Waliohojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM ni;
Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani,
Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu
Steven Wassira na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe.
Wengine ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema William Ngereja.
Hujuma dhidi ya Kinana zinakwenda mbali zaidi huku wasiwasi
ukitanda huenda hadi hujuma hizo kuweza kufanikiwa, Kinana atakuwa
amelipa gharama kubwa na hatima yake inaweza kuwa kitendawili kizito
siku za baadaye.
Chanzo cha habari cha uhakika kutoka kambi inayotajwa kuhusika
na hujuma hizo kinaeleza kwamba kinachomponza Kinana ni ujasiri
usiotarajiwa
alioonyesha kiasi cha kumudu kumshawishi Rais Jakaya Kikwete,
kuridhia awahoji ‘wagombea urais’, ikielezwa kwamba ujasiri wa Kikwete
binafsi si wa kiwango hicho hususan kwa wanasiasa wanaotajwa kuwa rafiki
zake.
“Kuna mambo kadhaa yanayomponza Kinana kwa sasa na kwa kweli
amekwishatambuliwa rasmi adui wa kambi mojawapo ya urais. Tangu achukue
nafasi ya Katibu Mkuu amekuwa akifanya ziara za kujenga chama mikoani,
ziara hizi zimepokewa vizuri kiasi cha si tu kumjenga Kinana kisiasa
lakini kukwamua haiba ya chama iliyofifia. Kwa hiyo, Kinana sasa anakuwa
kiongozi mwenye ushawishi zaidi si tu CCM bali hata katika kada
mbalimbali za kijamii, kuanzia wasomi hadi viongozi wa dini.
“Pili, hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kwenye
maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa Chama, Mjini Mbeya, kwa sehemu kubwa
alimsifu Kinana. Huu ni uthibitisho mwingine kwamba nguvu za Kinana
katika CCM ni kubwa sasa. Lakini kubwa zaidi linalomponza na mbali ni la
tatu ni kukataa kuwa na bei, hanunuliki wala kuhongwa na hapa kundi
fulani la urais kwa sababu linaamini katika nguvu ya fedha, Kinana ni
kikwazo kikubwa mno kwao,” kilieleza chanzo hicho cha habari.
Ni kutokana na hayo, chanzo chetu cha habari kinadokeza mambo
matatu yanayoweza kutekelezwa na kundi hilo dhidi ya Kinana na Mangula,
ambao ushawishi wa nguvu ya fedha kwao ni sawa na kile chanzo cha habari
kimeita “upuuzi”.
Mpango namba moja
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, mpango namba moja ni
kuunganisha nguvu kwa mawaziri walioitwa mizigo. Mawaziri hao wanapangwa
kujitokeza hadharani ili kumkabili Kinana, wakimlaumu katika mwelekeo
wa kumjengea chuki dhidi ya wanaCCM, kwamba amewadhalilisha bila kujali
kuitwa kwao mizigo msingi wake ni hoja za wananchi waliokutana na akina
Kinana katika mikutano ya hadhara.
Mpango namba mbili
Mpango namba mbili unatajwa kuwashirikisha baadhi ya wanasiasa
wa upinzani, ukilenga kutengeneza kashfa kwa gharama yoyote ile na
wanasiasa hao wa upinzani wazungumze mara kwa mara hadharani ili
kumvunja kasi Kinana. Tayari mwanasiasa mmoja ambaye ni mbunge kutoka
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema) anatajwa kuhongwa mamilioni
ili kutekeleza mpango huu.
Mpango namba tatu
Mpango namba tatu unatajwa kuwa ni wenye gharama kubwa zaidi kwa
Kinana. Mpango huu (hatuwezi kuutaja hapa) kama ukitekelezwa dhidi ya
Kinana na wahusika wakakamatwa na kufikishwa mahakamani basi, adhabu au
hukumu dhidi yao ni kunyongwa.
“Kwa hali ilivyo, kwao Kinana ndiye sasa mwenye ushawishi mkubwa
kuhusu nani mgombea bora wa urais kupitia CCM 2015 na kwa vyovyote
vile, wanashindwa kumshawishi kwa nguvu ya pesa. Amekuwa Katibu Mkuu
mwenye ujasiri unaowatia shaka katika malengo yao kisiasa,” kilieleza
chanzo chetu cha habari.
Kikao cha Maadili
Kuhusu kikao cha kamati ya maadili, inaelezwa kwamba baadhi ya
wagombea urais wamekuwa na hofu ya kuchafuliwa katika safari yao
kuelekea Ikulu 2015.
“Kinachowatia hofu ni kwamba kamati ya maadili adhabu yake
haikatiwi rufaa. Kwa mfano, mtu akipewa adhabu ya onyo tayari ni doa
kwake, akipewa onyo kali anafungiwa kugombea nafasi ya uongozi kwa miezi
sita. Akipewa karipio anafungiwa kugombea kwa miezi 12 na akipewa dhabu
ya karipio kali anafungiwa kugombea uongozi kwa miezi 18, hii inawatia
hofu sana na wanaamini Sna Mangula ni tatizo kwao,” alisema mtoa habari
wetu.
Kinana binafsi hakuweza kupatikana kuzungumzia hujuma
zinazopangwa dhidi yake. Na kwa upande mwingine juhudi za kuwapata
wahusika wa mpango huo hazijazaa matunda hadi sasa.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba kati ya wanaCCM waliowahi kupewa
adhabu ya karipio kali kutokana na utovu wa maadili ni mwanasiasa Thomas
Nyimbo, ambaye alifungiwa kugombea uongozi kwa miezi 18
HABARI KWA HISANI YA http://ccmchama.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment