Ndugu zangu,
Mambo
mengi yameendelea kuzungumzwa kuhusu marekebisho ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia kwenye mchakato wa kukusanya maoni,
mjadala wa rasimu ya kwanza na hata kwenye Bunge Maalum, watu wengi
wanazungumzia zaidi muundo wa Muungano - ama kuwa na serikali mbili kama
ilivyo sasa au kuwa na serikali tatu kwa maana ya kufufuliwa kwa
'hayati' Tanganyika.
Kila mmoja anasema lake analolijua, kwa utashi wake, si kuna uhuru wa kutoa maoni bwana!
Wanaotaka serikali mbili wana hoja, haziwezi kupuuzwa, na wanaotaka serikali tatu, nao pia wana hoja za msingi kabisa.
Inafurahisha kuona hoja za pande zote, na hasa nikiwa Mtanzania mwenye kupenda kupima mambo kabla ya kuyazungumzia.
Wanaotetea
serikali mbili, ambao wengi ni wa Chama cha Mapinduzi, wanahisi kwamba
kama Tanganyika itafufuliwa basi Muungano utakufa kibudu!
Lakini
wanaotetea kufufuliwa kwa Tanganyika ndani ya Muungano, wakiwemo
Wazanzibari ambao ndio wako mstari wa mbele kutaka kuona serikali-mwenza
ya muungano huo, wanaamini haki na demokrasia itatendeka ikiwa
Tanganyika itakuwepo. Kama kuna agenda nyingine ya siri kwa Wazanzibari,
hakuna anayejua zaidi ya shaka tu ya CCM.
Binafsi
NAUNGANA na wale wote wanaotaka serikali tatu, kwa sababu hakuna ndoa
ya upande mmoja! Kama Zanzibar wanayo serikali kwenye Muungano, basi
Tanganyika nayo inapaswa kuwa na serikali yake.
Kimsingi,
watu wasibezane, kwa sababu kinachotafutwa ni kutengeneza Katiba ya
Tanzania miaka 50 ijayo, watu wasifikirie maslahi yao ya sasa, bali
wanapaswa kuwafikiria watoto na wajukuu zetu.
Jambo
muhimu ni kwamba, Rais Jakaya Kikwete na serikali yake wanapaswa
kutumia hekima na busara katika suala hili kwa sababu ndilo pekee ambalo
linaweza ama kudumisha umoja na mshikamani pamoja na amani au linaweza
kuvuruga kabisa ikiwa uamuzi utakuwa wa kufuata utashi wa makundi.
Katika
kipindi ambacho serikali inatuhumiwa na kusimangwa kwa rushwa
iliyokithiri, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka, kukosekana kwa
uzalendo na kumong'onyoka kwa maadili ya uongozi, hakika Katiba Mpya
ndio urithi (legacy) pekee ambao Rais Kikwete atakapotoka madarakani
mwaka 2015 atakuwa amewaachia Watanzania.
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0715 070109
No comments:
Post a Comment