Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, March 19, 2014

SHEIKH PONDA AKWAMA MAHAKAMA KUU

  Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda anayekabiliwa na kesi ya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro na kukaidi amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akirudishwa rumande baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali maombi yake ya marejeo dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro. Picha na Michael Matemanga 
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda amekwaa kisiki mahakamani baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali maombi yake ya marejeo dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Sheikh Ponda anakabiliwa na kesi ya jinai namba 128 ya mwaka 2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, akikabiliwa na mashtaka ya kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro na kukaidi amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Sheikh Ponda kupitia kwa Wakili wake Juma Nassoro aliwasilisha maombi ya marejeo Mahakama Kuu, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kutupilia mbali maombi yake ya kumfutia shtaka la kukaidi amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katika amri hiyo iliyotolewa Mei 9,2013 na Hakimu Mkazi, Viktoria Nongwa, Ponda aliamriwa kulinda amani na kutokutenda kosa lolote kwa kipindi cha miezi 12, baada ya kumtia hatiani katika kesi ya jinai namba 245 ya mwaka 2012,iliyokuwa ikimkabili na wenzake 49.
Ponda kupitia kwa wakili wake aliiomba Mahakama hiyo imfutie shtaka hilo akidai kuwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shtaka hilo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro katika uamuzi wake uliotolewa, Oktoba Mosi, 2013, Hakimu Mkazi Richard Kabate anayesikiliza kesi hiyo, alitupilia mbali maombi hayo alisema mahakama hiyo inayo mamlaka ya kusikiliza shtaka hilo.
Ni uamuzi huo uliomsukuma Sheikh Ponda kupitia kwa Wakili wake Nassoro, kukimbilia Mahakama Kuu akiiomba ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, kinyume cha matarajio yake ya kupata unafuu, badala yake jana pia alijikuta akiangukia pua katika maombi yake hayo baada ya Mahakama Kuu kuyatupilia mbali.
Maombi hayo ya marejeo yalitupiliwa mbali jana na Jaji Augustine Mwarija aliyekuwa akiyasikiliza baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi lililowekwa na mkurugenzi wa mashtaka.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Mwarija alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusiana na pingamizi hilo, anakubaliana na hoja za Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo kinyume na Sheria.
Jaji Mwarija alisema kama Wakili Kongola alivyosema, kifungu cha 372 (2), kilichotumika katika maombi hayo kinazuia maombi ya marejeo ya uamuzi au amri iliyotolewa na mahakama za chini ambao haumalizi kesi ya jinai.
 MWANANCHI

No comments:

Post a Comment