Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, April 13, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUVUNJWA KABURI LA SHEIKH YAHYA HUSSEIN NA SHEIKH KASIM



Alhajj Maalim Hassan Yahya Hussein.
Ndugu Wanahabari,
Assalam Aleykum
Kama mnavyojua kwamba kumetokea tukio la kusikitisha  la kuvunjwa kwa Makaburi ya Masheikh Wetu, wapendwa wetu,  wazazi wetu na viongozi wetu wa Dini  ya Kiisalam, Marehemu Sheikh Yahya Hussein Na Marehemu Sheikh Kassim Bin Juma, Usiku wa kuamkia tarehe 10/4/2012 katika viwanja vya Makaburi ya Tambaza Jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Tukio hili, licha ya kusikitisha lakini limeziingizia fedheha  Familia hizi mbili za Masheikh Hawa na Kwa Waisalamu kwa Jumla. Kwa Desturi na Sheria, Viwanja vya Makaburi ni mahala panapotakiwa Kuheshimiwa kutokana na ukweli kwamba ni moja wapo ya sehemu za Ibada.
Hivyo basi kutokana na Tukio hilo ni dhahiri kwamba waliofanya kitendo hicho wamekiuka mafundisho ya Dini ya Kiislamu  na hivyo kutenda kosa ambalo kiimani linaweza kusababisha Madhara Makubwa kwao wenyewe, Jamii na Taifa kwa Jumla.
Kwa muktadha huo basi Familia ya Marhum Sheikh Yahya Hussein imeumizwa kwa kiwango cha juu na tukio hilo hasa ikizingatiwa kuwa  Makaburi yaliyovunjwa ni la baba yetu na la aliyekuwa swahiba wake  mkubwa Mzee wetu Sheikh Kassim Bin Juma Pekee.
Hali hii inaonyesha kwamba kuna Chuki Binafsi, Udhalilishaji na Njama  za Kuhujumu familia yetu, Dini yetu na Waislamu kwa Jumla na hivyo kitendo cha aina hii kinaweza kuliingiza Taifa katika migogoro isiyo na Tija, kidini, Kisiasa, kiuchumi na kimaendeleo ya Jamii.
Hata hivyo Familia ya Marhum Sheikh Yahya Hussein imefarijika kuona uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dar es salaam  Pamoja na Baraza Kuu La Waisalamu wa Tanzania (BAKWATA) chini ya Mufti wa Tanzania Sheikh Mkuu Issa Bin Shaaban Simba kulishughulikia kwa haraka suala hili katika mawanda ya kuthamini, Mila, Desturi na Ibada za Makaburi.
Hatua hiyo inaonyesha ni jinsi gani Jamii nzima ilivyoguswa na kadhia hiyo ambayo inahatarisha Usalama wa Nchi na raia kwa sababu Waumini na wananchi wengine ambao ni wapenzi wa Viongozi hao wa Kidini wanaweza, kutokana imani zao, kujichukulia sheria mikononi.
Hata hivyo uongozi wa Serikali Mkoa wa Dar es salaam na vyombo vyake bado unatakiwa kuwa makini katika maagizo yake na utekelezaji wa kazi zake hasa katika sehemu ambazo zinagusa hisia za watu kama Makaburi na sehemu za Ibada ili kuepuka matukio yenye sura ya Hujuma kama tukio hilo la makaburi ya Tambaza ambayo yanaweza kuleta mtafaruku ndani ya jamii na kuvunjika Amani ya nchi.
Sisi kama Familia Ya marehemu Sheikh Yahya Hussein tunaiomba Serikali na vyombo vyake iwasake na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliohusika na hujuma hizi.
Pamoja na hayo familia inaona kwamba dawa ya kuepukana na matatizo kama haya ni kujenga uzio katika eneo hilo ili kuhifadhi Makaburi hayo. Kwa hiyo tunaiomba Manispaa ya Wilaya ya Ilala ijenge uzio katika  eneo la Makaburi ya Tambaza.
Kwa upande wetu, pamoja na nia nzuri ambayo Serikali imeonyesha ya kutaka kuyajenga tena Makaburi hayo, lakini sisi kama Familia ya Sheikh Yahya Hussein na Sheikh Kassim Bin Juma tumeamua kwamba tutajenga Makaburi  ya wazazi wetu kwa gharama zetu wenyewe.
Wabillahi Tawfiq
Alhajj Maalim Hassan Yahya Hussein
( Kwa niaba ya Familia)

No comments:

Post a Comment