skip to main |
skip to sidebar
MWANAMKE KUWA MAKINI NA MWANAUME MWENYE TABIA HIZI HAWAFAI.
1. Mwanaume Kicheche:
Hakuna mwanamke anayependa kuchezewa na wanaume, labda tu kama anafanya
hivyo katika juhudi zake za kujikwamua kiuchumi, lakini pale mwanamke
anapokuwa katika harakati za kutafuta mwanaume ambaye kama mambo yakiwa
mazuri wafunge ndoa, ni vyema akajiepusha na wanaume vicheche
wanaotongoza wanawake kwa lengo la kustarehe na kumaliza matamanio yao
ya ngono. wakati mwingine mwanaume mwenye tabia ya kuchezea wanawake
anaweza kumfuata mwanamke ambaye ametamani mwili wake na kujifanya eti
amebadilika na kuwa mtakatifu. Anaweza kujiweka katika mazingira
yanayoonyesha kwamba amebadilika ili kumvuta mwanamke. Shituka mwanamke,
jasiri haachi asili atakutumia kama condom na kisha kukutupilia mbali.
Wanaume wenye tabia hizo ni vigumu kubadilika. Inahitaji subira ya hali
ya juu kujiridhisha kama kweli amebadilika au anazuga ili apate
anachokitaka.
2. Mwanaume asiye na kazi na asiyejishughulisha:
Mwaume asiye na kazi na asiyejishughulisha ni mzigo usio na mwenyewe.
Mwanaume asiyejishughulisha eti kwa sababu hajapata kazi huyo hana
malengo. Kukubali kuwa na uhusiano na mwnaaume wa aina hiyo ni sawa na
kuishi na mtu mfu anayetembea (dead alive), labda tu kama atakupa sababu
inayoingia akilini kuhusu kutokuwa kwake na kazi na kutojishughulisha
kwake. Kama atakuwa ni mtu wa kulalamika tu kwamba hakuna ajira na
haonyeshi dalili zozote za kuhangaika kutafuta hata vibarua ili kujikimu
eti kwa sababu ni msomi na badala yake anageuka kuwa ombaomba kwa ndugu
zake na marafiki zake Nawashauri wanawake muwaepuke wanaume wa aina hii
kwani hawafai wanataka kulelewa. Kama amekuona unafanya kazi au una
vibishara vyako vinavyokuingizia shilingi mbili tatu zinazokufanya uishi
vizuri hapa mjini jua kwamba hicho ndicho kilichomvuta kwako, ukikubali
umekwisha maana atakukamua hadi tone la mwisho kisha ahamie kwa
mwingine, si kilichomleta kwako hakipo, sasa awe na wewe kwa lipi....
3. Mwanaume asiyejiamini:
Kukubali kuwa na mahusiano na mwanaume asiyejiamini ni sawa na kuishi na
bomu ndani ya nyumba. Mwanaume asiyejihisi kuwa yuko salama na mwenye
mashaka muda mwingi kuhusu uhusiano wenu, hutawaliwa na wivu wa ajabu
ambao licha ya kukuletea fedheha kwa ndugu, jamaa na marafiki zako,
lakini pia anaweza kukudhuru au hata kukutoa roho siku moja. Wanaume
wasiojiamini mara nyingi ni watu wa kujitilia mashaka kuhusu hali zao za
kipato na uwezo wao katika tendo. Kuwa na mahusiano na mwanaume
asiejiamini inabidi uishi kwa akili na uchague maneno ya kuzungumza kila
uwapo naye, kwani kila neno utakalotamka litatafutiwa tafsiri na
kitakachofuata ni tafrani, sasa tabu yote ya nini..... Tupa kule hafai
kwa mchuzi wala kwa kulumangia...
4.Mtoto wa mama:
Inawezekana mwanaume akalazimika kuishi nyumbani kwao kwa muda baada ya
kumaliza masomo au amepoteza ajira na akawa bado hajapata ajira au
hajapata shughuli ya maana itakayomwezesha kujitegemea, hii inakubalika.
Hata hivyo kama mwanamke anakutana na mwanaume ambaye anaishi na wazazi
wake na haonyeshi dalili za kutafuta kazi au shughuli yenye kipato
itakayomwezesha kuondoka hapo kwao na kujitegemea, usije ukajiingiza
katika uhusiano na mwanaume wa aina hiyo, itakula kwako, huyo ashakuwa
kupe na tegemezi, utakuwa ni mzigo wako na atakuganda kama luba na
kupoteza bahati ya kukutana na wanaume wenye mwelekeo wa maisha.
5. Mwanaume anayependa kutukuzwa kama mfalme:
Unaweza kukutana na mwanaume aliyejipachika kibandiko ufalme ambaye
anapenda sana kuhudumiwa kama mfalme. Yaani anataka afanyiwe kila kitu,
na hajishughulishi kukusaidia kazi hata zile zinazotakiwa zifanywe na
mwanaume, yeye kazi yake ni kukaa sebuleni na kuangalia TV au kusoma
vitabu au magazeti huku akiagiza kila kitu asogezewe miguuni. Hawezi
hata kunyanyuka kufuata kitu anachotaka na badala yake ni kuamrisha
aletewe. Mwanaume wa aina hii ni wa kuepukwa kwani mwanamke kukubali
kuwa na uhusiano na mwanaume mwenye tabia za kupenda kutukuzwa kama
mfalme ni kutaka kuishi kwa msongo wa mawazo na jakamoyo na hivyo
kufupisha umri wako wa kuishi hapa duniani. Kinga ni bora kuliko tiba,
ukikutana na mwanaume wa aina hii chapa lapa hakufai..
6. Mwanaume mwenye utititri wa watoto kila kona:
Mwanaume kuwa na watoto nje ya ndoa si jambo la kushangaza siku hizi,
lakini pale unapokutana na mvulana mwenye umri wa miaka 25 lakini ana
watoto watatu kwa mama tofauti, mh! hapo sikushauri ujiingize kwenye
uhusiano na mwanaume huyo. Hata hivyo si lazima awe na miaka 25 tu hata
mwanaume mwenye umri mkubwa zaidi ya huo halafu ana watoto watatu au
hata wanne au zaidi kutoka kwa mama tofauti ni wa kuepuka. Hivi atakupa
sababu gani zilizomfanya akawa na watoto kwa mama tofauti kila kona ya
mtaa mpaka umuelewe! Kuwa na mahusiano na mwanaume aina hiyo ni
kukaribisha shari nyumbani kwako maana kila siku utapata wageni
wanaokuja kudai hela za matumizi kutoka kwa mumeo tena wengine watakuja
kishari hasa na kukuharibia siku. Mh mh! sikushauri mwanamke, sepa zako,
bado nafasi unayo ya kumpata mwanaume mwingine mwadilifu.
7. Mwanaume anayejipenda mwenyewe:
Mwanaume anayejipenda mwenyewe ni kizungumkuti kingine ambacho wanawake
wanapaswa kujiepusha nacho. Utakuta mwanaume anajipenda mwenyewe hakuna
anachojali kuhusu mwenzi wake zaidi ya kujijali yeye mwenyewe. Wanaume
wenye tabia hii ya kujipenda wenyewe, huwa wana kawaida ya kujijali wao
wenyewe. Wanataka wavae nguo nzuri za thamani ili wao wapendeze na si
wenzi wao. Swala la kumjali mwenzi wake halipo katika vichwa vya wanaume
wa aina hii kabisa. Mwanamke sikushauri uingie katika moto huu.
8.Mwanaume bahili:
Unakutana na mwanaume mtoko wa kwanza tu anakuchagulia aina ya chakula
au kinywaji kwa kuangalia bei rahisi na wakati wa kulipa anahesabia hela
yake mfukoni, huyo ni janga. Utakapoingia katika uhusiano na mwanaume
wa aina hii atakusumbua sana na pia katika kupanga bajeti nyumbani
usishangae akihesabu finyango za nyama au vipande vya samaki jikoni.
Sikushauri mwanamke, we ingia mitini hakufai huyo........
9.Mwanaume chapombe mlevi kupindukia:
Hakuna ubaya mtu kunywa pombe, hasa kama unajua kiwango chako cha
unywaji, lakini kuwa na uhusiano na mwanaume mlevi anayekunywa pombe
kupindukia kila siku non stop 24/7 huyo hafai. Mwanaume wa aina
hii ndio wale wanaosema kunywa pombe watoto wakitembea uchi atajua mama
yao. Hata siku moja hawezi kuzungumzia maendeleo kwa ustawi wa familia,
kwake utakuwa ni msamiati mgumu.
10. Mwanaume mwenye kisirani na asiyeweza kumuuwa nyoka akafa :
Mwanaume mwenye kisirani ni ngumu sana kuishi naye. Mwanaume mwenye
kisirani na anayependa kuweka vitu rohoni na asiyeweza kusamehe ni
janga. kuishi na mwanaume wa aina hii ni sawa na kuishi na explosive material ambayo
yakipata joto tu hulipuka. Mwanaume umetoka naye mtoko wa kwanza na kwa
bahati mbaya mhudumu wa mghahawa akasau kitu katika vitu mlivyoagiza
akagomba kupita kiasi na kuwakusanya mameneja wote wa mghahawa akiwemo
mpishi mkuu akilalamika. Na kama hiyo haitoshi mtaondoka hapo mghahawani
njia nzima kambeba kichwani mhudumu yule masikini aliyeghafilika mpaka
mwisho wa safari yenu na huenda akalala naye kichwani. Mwanaume huyo
hafai kama gome la mgomba lisilofaa kwa dawa ya miti shamba wala kuni,
labda kwa kufungia ugoro. Huyo mpishe ajiendee zake hakufai......
No comments:
Post a Comment