SERIKALI ya Tanzania kupitia vyombo vyake inakusudia
kuwashitaki waliohusika na nyaraka zinazohofiwa za kughushi zilizotumika katika
mauzo ya hisa za kampuni ya kufua umeme ya Independet Power Limited (IPTL),
hatimaye kuchukua fedha zilizohifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika
akaunti maalumu ya pamoja (ESCROW).
Taarifa za ndani ya serikali zilizonaswa zinaeleza kwamba
hatua hiyo inafuatia mkanganyiko wa nyaraka zilizowasilishwa serikalini
kuonyesha kwamba asilimia 70 ya hisa za IPTL zimeuzwa katika mazingira tata na
kufanikishwa kuchukuliwa kwa mamilioni ya shilingi kutoka BoT.
Tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) wamepokea nyaraka
zinazohusu sakata hilo kabla ya maamuzi kufanywa kuhusu ni watu gani
watakaofikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baadhi ya watuhumiwa ni raia wa
kigeni na baadhi wakiwa ni Watanzania ambao ni watendaji ndani ya serikali na
taasisi zake.
Mauzo ya IPTL yaliyoidhinishwa na Wizara ya Nishati na
Madini, yalisababisha BoT kuruhusu kuchukuliwa kwa takriban Sh bilioni 200
(Dola za Marekani milioni 122) zilizokuwa zimehifadhiwa kusubiri kwisha kesi kati
ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
imeelezwa kwamba fedha hizo zililipwa muda mfupi kabla ya
mitambo ya IPTL kuwa mali ya Tanesco, kukiwa na ushauri wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano kusubiri.
Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari na katika mitandao
Ya Jamii zinaeleza kwamba kuna utata kuhusiana na kinachotajwa kuwa ni mauzo ya
sehemu kubwa ya hisa (70%) za IPTL zilizokuwa zikimilikuwa na kampuni ya
Mechmar ya Malaysia kwenda kampuni ya Piperlink limited ya British Virgin
Island kwa bei ya shilingi milioni sita za Kitanzania.
Kupitia mchango wake bungeni na barua kwenda kwa CAG, Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe, ambaye ametaka vyombo hivyo kufanya
uchunguzi na kufanya maamuzi sahihi na ya haki ili fedha za umma zisipotee
katika mchango wake wa Bajeti ya Serikali ya mwaka huu aliouwasilisha kwa
maandishi, Zitto amezungumzia IPTL kwa kusema:
“Hisa za kampuni ya Mechmar (ndani ya IPTL) 'ziliuzwa' kwa
kampuni ya Piperlink Limited ya British Virgin Island kwa bei ya Shilingi za
Tanzania milioni sita. Kwa hiyo kodi ya
ongezeko la mtaji iliyolipwa TRA ni ya thamani hiyo. Kampuni hiyo ya Piperlink
limited nayo ikauza hisa zake kwa kampuni ya PAP kwa bei ya dola za Marekani
300,000.
“Malipo ya kodi kwa kampuni zote ( Mechmar na Piperlink)
yalifanywa siku moja tarehe 6 Disemba 2013 siku moja baada ya kampuni ya PAP
kulipwa fedha za Tegeta Escrow (iliyopo BoT). Nyaraka zote zinaambatanishwa
hapa.”
Zitto amesema katika mchango wake huo wa maandishi kwamba
Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 kifungu cha 29 inataka kwanza kodi kulipwa kabla
ya mamlaka za ruhusa kutoa ruhusa kwa uuzaji wa hisa kutoka mmiliki wa zamani
kwenda mmiliki mpya.
“Nyaraka hizi zinaonyesha kuwa kampuni ya PAP iliingia
mikataba na mamlaka za Serikali bila ya kuwa na umiliki wa kampuni ya IPTL. Pia
ni dhahiri kampuni hizi za Mechmar, Piperlink na PAP zilikwepa kodi kwa
kuuziana hisa kwa bei ya chee ili walipe kodi kidogo. Iweje hisa 70% za Mechmar
ziuzwe kwa shilingi milioni sita wakati kampuni ina mtambo, ardhi na akiba
Benki Kuu na Tanesco ya thamani ya jumla ya dola za Marekani 250m?” alihoji
akitaka Waziri wa Fedha kutoa maelezo kuhusiana na suala hilo.
Kabla ya kuwasilisha bungeni maelezo hayo kwa maandishi,
Zitto aliwasilisha barua kwa CAG Juni 19 mwaka huu, akiomba uchunguzi mpya wa
fedha zilizotolewa BoT kutoka akaunti ya Escrow katika mazingira tata.
Zitto katika barua yake kwa CAG amesema ni dhahiri mpango
mzima wa kuchukua fedha za Escrow ulichorwa na mtandao mpana ndani ya Serikali
na kumtaka CAG kufanya uchunguzi wa kina na kutoa taarifa ambayo itaanika
ukweli kuhusu sakata hilo.
“Utakumbuka kwamba Kamati ya PAC ilikuomba ufanye uchunguzi
kuhusu uhalali wa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta kulipwa kwa kampuni
ya Pan Africa Power Solution (PAP). Napenda kukuletea nyaraka muhimu sana
zikusaidie kwenye uchunguzi wako ili kubaini ukweli wa jambo hili.
“Nakuletea barua ya TRA yenye kumbukumbu nambari
TRA/DR/ILA/RE/175 ya tarehe 15/11/2013 ambapo inaonyesha kuwa kampuni ya
Mechmar ya Malaysia iliuza hisa zake asilimia 70 katika kampuni ya IPTL kwa
kampuni ya PiperLinks Investment Limited mnamo tarehe 9/9/2013 kwa thamani ya
Tshs 6,000,000.00,” anasema katika barua yake kwa CAG.
Amesema kwamba nyaraka za malipo ya kodi zinaonyesha Mechmar
walilipa kodi ya ongezeko la mtaji Sh. 596,000.00 na kodi ya stempu ya Sh.
180,000.00 Desemba 6 mwaka 2013 katika Benki ya CRDB Waterfront Branch.
“Kampuni ya PiperLinks nayo iliuza hisa zake kwa Kampuni ya
Pan Africa Power Solutions mnamo tarehe 30 Oktoba, 2013. Barua ya TRA
inaonyesha kuwa kodi iliyolipwa ni kodi ya ongezeko la Mtaji tshs 47,940,000.00
na ushuru wa stempu tshs 4,800,000.00. Malipo ya kodi hiyo yalilipwa siku ile
ile ambayo Mechmar walilipa, tarehe 6 Desemba 2013,” anasema.
Zitto amesema katika barua yake hiyo kwamba hata amri ya
Mahakama ilipotolewa kuwa PAP wapewe mali za IPTL, kampuni hiyo haikuwa na
umiliki wa wowote wa IPTL.
“Katika nyaraka ninazokuletea kuna ushahidi wa kutosha
kabisa kwamba hapakuwa na uhamishaji wa umiliki wa hisa za IPTL kwa PAP kwani
ni dhahiri nyaraka zote zilizowasilishwa na PAP serikalini zilikuwa ni nyaraka
za kughushi.
“Katika uchunguzi wako ni muhimu pia nyaraka za PAP
zichunguzwe uhalali wake. Kwa mfano, TRA hawana hati halisi za hisa za IPTL
ambazo ziliwasilishwa na PAP ili kuthibitisha umiliki wao. Pili, utaona kuwa
iweje kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa na hisa 30% katika IPTL ilipwe dola
za Marekani milioni 75 wakati Mechmar iuze asilimia 70 kwa tshs milioni 6 tu na
PiperLink iuze kwa dola laki tatu tu? Halafu mali mojawapo ya IPTL iliyolipwa
kwa PAP ni dola za Marekani milioni 122?” anahoji Zitto.
No comments:
Post a Comment