Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Msaidizi wake, wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya
matumizi mabaya ya madaraka.
Washitakiwa hao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe
pamoja na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, Hamad Koshuma.
Walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na
Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincolin
akisaidiana na Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekoma.
Wakili Lincolin alidai kuwa Desemba 5 mwaka 2011 katika
ofisi ya Mamlaka ya Bandari, washitakiwa wakiwa waajiriwa wa mamlaka hiyo,
walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mkataba na Kampuni ya China
Communication Contraction.
Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao, walisaini mkataba huo kwa
ajili ya ujenzi wa Geti Namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam, bila
kutangaza zabuni, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na lilikuwa na lengo la
kuinufaisha kampuni ya China.
Washitakiwa walikana kutenda makosa hayo na kuachiwa kwa dhamana baada ya
kutimiza masharti ya kusaini hati ya Sh milioni mbili pamoja na kuwa na
wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni mbili.
Upande wa mashitaka ulidai upelelezi bado haujakamilika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 13 mwaka huu, itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment