Flora Nathaniel Shayo (60) mkazi wa Chanika, wilayani Ilala,
Dar ameiomba serikali pamoja na Rais Jakaya Mrisho Kikwete imsaidie baada ya
kukatwa miguu kutokana na kuugua ugonjwa wa kisukari.
Akizungumza na waandishi wetu hivi karibuni, Flora alisema
aliwahi kuwa muuguzi (nesi) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa miaka 26
iliyopita na baada ya kustaafu alikuwa akifanya biashara ya kuuza dawa za
binadamu (Duka la dawa) huku mwanaye akiwa anafanya kazi za muziki. Mama huyo
aliendelea kufunguka kuwa, aligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari na presha
mwaka 2006 ndipo akaanza kutumia dawa.
CHANZO CHA UGONJWA
Akifafanua zaidi mama huyo alikuwa na haya ya kusema: “Mwaka
2011 kidole gumba cha mguu wangu wa kulia kilianza kukauka na kubadilika rangi
nikaenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Nilipofika hospitali nilipimwa na kugundulika kuwa sumu
imepanda mpaka juu karibu na goti, madaktari wakaniambia ni lazima nikatwe mguu
ili kuokoa maisha yangu. Nilipatwa na woga, lakini sikuwa na la kufanya,
nilikubali.
“Nikaandaliwa na kupelekwa katika chumba cha upasuaji na
kukatwa mguu, nilikuwa siamini kama kweli nimekuwa kilema lakini ilinibidi
niamini, kweli hujafa hujaumbika,” alisema mama huyo huku akiwa na majonzi.
“Tangu nimekatwa mguu wa kwanza nateseka, mwanagu Dogo
Mfaume ambaye ni mwanamuziki hana uwezo wa kunisaidia kutokana na ukweli kwamba
hana kipato cha kutosha,” alisema huku akilengwalengwa na machozi.
Flora Nathaniel Shayo kabla ya kukatwa miguu.
AKATWA MGUU WA PILI
Akasema: “Haukupita muda mrefu mguu wa pili nao ukaanza
kuvimba, nilihisi kuchanganyikiwa na nikaona kuwa huo sasa ndiyo mwisho wa
maisha yangu.
“Kwa kweli nilipatwa na msongo wa mawazo na kukata tamaa ya
kuendelea kuishi baada ya kwenda tena Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na
madaktari kuniambia mguu wa pili nao ukatwe, nilikatwa, namshukuru Mungu
nimeuguzwa na kidonda kilipona vizuri lakini baada ya hapo nahisi akili yangu
ilihama kabisa maana nilikuwa nahesabu siku za kuishi tu.
“Hakika mganga hajigangi. Sion thamani ya kuishi hapa
duniani, nimebaki mkiwa na kujiona nastahili kufariki dunia maana sijui hata
muelekeo wa maisha yangu utakuaje.”
OMBI KWA WATANZANIA
Baada ya kujifuta machozi kwa kanga yake aliendelea kusema:
“Nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie kunichangia ili niweze kupata kiti cha
magurudumu (wheelchair) kitakachoniwezesha kutoka nje na kufanya shughuli
zangu.
“Ikiwezekana wanisaidie nipate miguu ya bandia, maana
nashindwa hata kwenda nyumba ya ibada kusali au kufanya shughuli ndogondogo
wakati bado nina nguvu kabisa ya kujitafutia riziki na kujenga taifa langu.”
OMBI KWA RAIS
Alimgusa Rais Kikwete huku akitiririka machozi akasema:
“Namuomba Rais Kikwete aniangalie kwa kuwa nilifanya kazi Muhimbili kwa muda
mrefu na pesa niliyoipata baada ya kustaafu haikuweza kukimu mahitaji yangu
mpaka sasa nimebaki kama yatima tu.
Akikabidhiwa cheti baada ya kuhitimu kozi ya unesi.
“Watoto wangu hawana
uwezo na msaada nilioupata hospitali ni wa matibabu tu pale nilipohitajika
kukatwa mguu, nahitaji dawa za kila siku, chakula na mahitaji mengine na dawa
za kisukari ni gharama sana, kuna wakati nakosa hata pesa ya kununulia kwani
presha pia inanisumbua.”
ATOA NENO KWA WASANII
“Kwa kuwa mwanangu Dogo Mfaume ni msanii, nawaomba rafiki
zake na wasanii wenzake wanisaidie kwani hali niliyonayo ni mbaya, mpaka sasa
naishi tu kwa matumaini. Kuna siku nakosa hata hela ya kwenda kujitibu,”
alisema mama huyo kwa uchungu.
Naye Dogo alipotafutwa kuzungumzia ishu hiyo alisema, kwa
sasa mambo yake hayapo sawa ndiyo sababu anashindwa kukidhi mahitaji ya mzazi
wake.
“Kusema kweli hali ya mama inaniumiza sana kichwa, nashindwa
hata kuelewa cha kufanya, nashindwa kumudu mahitaji yake ipasavyo ni tatizo
kikubwa ningependa kwa yeyote ambaye yupo tayari kumsaidia basi asisite, siku
zote mimi namuombea kwa Mungu mzazi wangu,”alisema Dogo Mfaume.
Yeyote aliyeguswa na habari hii na angependa kumsaidia
awasiliane na mama huyu kwa namba 0755
216 865, kutoa ni moyo, sioyo utajiri.
No comments:
Post a Comment