Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema kuwa litaendelea kuwabana wafanyabiashara wanaoingiza nguo za mitumba za ndani zilizopigwa marufuku ili kuhakikisha kwamba biashara hiyo inakoma nchini.
Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa shirika hilo, Rhoida Andusamile jijini Dar es Salaam.
Andusamile alisema wapo wafanyabiashara ambao sasa wanafanya ujanja wa kuchanganya nguo za mitumba za kawaida na za ndani ili zisionekane kuwa zimo zilizopigwa marufuku.
Alisema kuwa katika ujanja huo, wafanyabiashara wanaoingiza marobota wamekuwa wakizichanganya nguo kwa ufundi ili zionekane za aina moja huku wakiwa wameweka nguo za ndani za kike na kiume zilizopigwa marufuku.
"Tunapobaini hilo huwa tunaziteketeza na tunaendelea kufanya hivyo kadiri inavyowezekana ingawa kwa sasa wapo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanaotumia njia za panya kuingiza bidhaa hizo nchini," alisema.
Alisema kuwa sasa wanatumia njia za panya baada ya kubanwa bandarini na maeneo mengine yakiwamo ya mipakani, hali ambayo kwa kiasi imepunguza wingi wa uingizwaji wa nguo hizo.
Alisema kuwa shirika hilo limekuwa likiwafuata wafanyabiashara hadi kwenye maghala wanayohifadhia marobota ya nguo hizo na kufanya ukaguzi wa kina na wanapobaini kuwapo kwa nguo zilizopigwa marufuku huziteketeza.
"Mwanzoni wakati zoezi la kuondoa nguo hizo sokoni, walikuwapo wafanyabiashara waliodai kuwa wana mzigo mkubwa wa nguo hizo wakaomba wapewe muda ili waumalizie, lakini ajabu ni kwamba wanaendelea kuingiza nchini kinyemela," alisema.
Alisema kuwa TBS imeshagundua ujanja huo na ndiyo maana imekuwa ikiwafuatilia kila kona ili kuhakikisha kwamba wanaacha kuingiza nguo hizo ambazo kimsingi hazifai kuvaliwa.
Andusamile alisema kuwa hatua ya kuondoa nguo hizo sokoni ni utekelezaji wa matakwa ya agizo la Sheria ya 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani zilizokwisha kutumika.
Alisema kuwa licha ya unafuu wa gharama za upatikanaji wa nguo hizo, shirika hilo litaendelea kusimamia sheria na kupambana na wauzaji soksi, nguo za kulalia, sidiria, chupi na nyingine nyingi za aina hiyo.
Hata hivyo, alisema bado ipo haja ya kutoa elimu kwa jamii ili kuepuka nguo hizo, kutokana na ukweli kwamba zimekuwa zikiwasaidia watu wengi hasa wale wa kipato cha chini ingawa jambo la msingi ni afya.
No comments:
Post a Comment