Pichani mtuhumiwa Hamis Mohamed (47) Mkazi wa Kondoa aliyekamatwa eneo la Mianzini jijini Arusha akiwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi iliyokuwa inasafirishwa toka nchi jirani ya Kenya kuelekea Kondoa mkoani Dodoma (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mtu mmoja aitwaye Hamis Mohamed (47) Mkazi wa Kondoa mkoa wa Dodoma, amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha baada ya kukutwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi aliyekuwa anaisafirisha kwa mtindo wa aina yake.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba tukio hilo lilitokea tarehe 05.11.2014 muda wa saa 11:00 jioni eneo la Mianzini ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa anasafirisha madawa hayo kwenye gari aina ya Fusso basi lenye namba za usajili T. 577 BFM ambapo aliihifadhi kwenye magunia mawili huku juu na pembeni ya magunia hayo akiweka viatu.
‘’Katika magunia yale alikuwa ameweka viatu na katikati aliweka viroba 36 vya madawa hayo aina ya mirungi ambayo alikuwa anasafirisha toka nchini Kenya kupeleka Kondoa mkoani Dodoma hivyo ukiangalia unaweza kusema ni viatu pekee’’. Alifafanua Kamanda Sabas.
Alisema tukio hilo lilifanikiwa kutokana na mahusiano mema yaliyopo kati ya Jeshi hilo na raia wema ambao walitoa taarifa iliyofanyiwa kazi haraka na asakari wa Jeshi hilo.
Baada ya askari hao kupata taarifa hiyo walianza kulifuatilia gari hilo na lilipofika maeneo ya Mianzini jijini hapa kwenye maegesho ya basi hilo ndipo walipoanza kufanya upekuzi na kufanikiwa kukamata magunia hayo yaliyokuwa na viatu vilivyochanganywa na madawa hayo.
Kamanda Sabas alisema kwamba mtuhumiwa huyo bado anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment