SERIKALI imesitisha ongezeko la tozo zilizoanza kutumika
hivi karibuni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo ndiyo yenye
vifaatiba na madaktari wenye uwezo mkubwa kuliko hospitali yoyote nchini.
Hatua hiyo ya Serikali, ipo katika kauli ya Serikali
bungeni, iliyotolewa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid,
ambapo pia Bohari ya Dawa (MSD) iliagizwa kupeleka dawa muhimu zenye thamani ya
Sh milioni 200 katika hospitali hiyo.
Hivi karibuni hospitali hiyo ilipandisha gharama za huduma
hospitalini hapo, ambapo mgonjwa aliyetakiwa kulazwa baada ya kupatiwa rufaa
kutibiwa katika hospitali hiyo, alipaswa kulipa Sh 5,000 kwa siku na Sh 2,000
za chakula, ambazo hazikuwepo hapo awali.
Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, ,
ilikaririwa na vyombo vya habari, ikieleza kuwa gharama mpya zilianza kutumika
Oktoba 17, mwaka huu.
Kutokana na gharama hizo, baadhi ya wahudumu hospitalini
hapo walikaririwa wakisema idadi ya wagonjwa imepungua wodini kutokana na wengi
wao kushindwa kumudu gharama.
Wagonjwa kutoka mikoani waliathirika zaidi, kwa kulazimika
kutafuta malazi nje ya hospitali hiyo, hata kama hali zao ni mbaya.
Aidha, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiuguza ndugu zao,
walikaririwa kuchukua uamuzi wa kuwarejesha nyumbani ili kukwepa gharama hizo.
Miundombinu
Mbali na kusitisha ongezeko hilo la tozo, Dk Seif pia
ameagiza uongozi wa hospitali hiyo kurekebisha mara moja mazingira na
miundombinu ya hospitali hiyo, ambayo yapo ndani ya uwezo wao.
Ingawa tamko hilo halikufafanua, lakini taarifa zinaonesha
kuwa hospitali hiyo ilikuwa ikizidiwa na wagonjwa, kiasi cha baadhi kulazimika
kulala sakafuni.
Vyombo vya habari viliripoti kuhusu hali ya usafi wa vyoo
vya wodi ya Sewa Haji kuwa mbaya, licha ya kuwapo taarifa za kutolewa kwa
zabuni kwa kampuni kadhaa kufanya usafi, unaokidhi viwango na kanuni za afya
bora.
Baadhi ya vyoo havikuwa na maji na vifaa vya kusukuma maji
havikuwa vikifanya kazi, huku baadhi ya mabomba yakiwa na kutu.
Kutokana na ukosefu wa maji, wagonjwa na watu
wanaowatembelea, alilazimika kutumia maji yaliyopo kwenye mapipa nje ya vyoo na
yalipokosekana, walitafuta mahali kwingine ikiwamo nje ya jengo hilo.
Baadhi ya vyombo vya habari, viliripoti kushuhudia baadhi ya
vyoo vikiwa vimejaa uchafu katika majengo ya Sewa Haji, Kibasila na Mwaisela
huku vingi vikiwa katika hali mbaya ya uchakavu, kutokana na kutumika muda
mrefu bila kufanyiwa ukarabati.
Deni MSD
Kuhusu deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Dk Rashid alisema
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha ilifanya
uhakiki wa deni la MSD la Sh bilioni 41.5.
Baada ya deni hilo kuhakikiwa, alisema Serikali ilianza
kulipa kwa awamu ambapo Sh bilioni 8 zililipwa Juni 14, Sh bilioni 2 Agosti na
Sh bilioni 20 zimelipwa mwezi huu. Alisema kiasi kilichobaki cha Sh bilioni
11.5, kitalipwa mwezi ujao.
Kuhusu kutenga fedha za kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi kupitia MSD ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata dawa na
vifaa tiba kwa wakati, alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Bunge
liliidhinisha Sh bilioni 70.5 kwa ajili ya kazi hiyo. Ocean Road Akizungumzia
huduma za afya katika Hospitali ya Ocean Road, alisema huduma za matibabu ya
saratani inaendelea kutolewa,
kutokana na mashine ya E80 kuendelea kufanya kazi na kwa
sasa ndiyo inayotibu wagonjwa wote wa saratani katika taasisi hiyo.
"Kutokana na kuwepo kwa mashine moja tu ya mionzi
inayofanya kazi, kwa sasa hivi mashine inafanya kazi kwa saa 18 kwa siku ili
kupunguza mlundikano wa wagonjwa.
"Mashine ya intra cavitary ambayo ilikuwa imesimama
kufanya kazi kutokana na ubovu na kukosekana kwa vifaa muhimu, imetengenezwa na
sasa imeanza kufanya kazi hivyo kuwezesha matibabu ya wagonjwa wa saratani ya
shingo ya kizazi kwa ufanisi zaidi," alisema Waziri.
Nafasi ya Njelekela yatangazwa
Wakati hali ikiwa hivyo, nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Muhimbili, ilitangazwa jana kuwa iko wazi. Sifa za mtu anayetakiwa kujaza
nafasi hiyo ni pamoja na Shahada ya Uzamili katika Udaktari wa Binadamu; au
sifa inayolingana na hiyo katika masuala ya udaktari na upasuaji, pamoja na
uzoefu wa zaidi ya miaka kumi katika uongozi wa hospitali.
Tangazo hilo lilitolewa na hospitali hiyo na lilikuwa katika
gazeti la Daily News la jana, Ukurasa wa Nne. Waombaji wenye vigezo
vinavyotakiwa, wanatakiwa watume maombi ya kazi hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa Hospitali.
No comments:
Post a Comment