Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, November 5, 2014

Yaliyojiri Bungeni Dodoma: Leo Jumatano, Tarehe 05 Novemba, 2014



Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai

Leo ikiwa ni tarehe 5 Novemba, 2014, Kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), Kikao cha pili, mkutano wa 16 / 17.

- Kikao cha bunge leo kimeongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai.

- Hati za kuwasilisha mezani ni kutoka Wizara ya fedha, Ofisi ya Rais, na Kambi ya Upinzani.

- Naibu Waziri wa fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba alianza kwa kuwasilisha hati za Wizara ya fedha mezani.


- Waziri wa nchi, ofisi ya Rais Sera na uratibu, Stevene Wassira amewasilisha pia hati ya mpango wa maendeleo.

- Kambi ya Upinzani, nayo imewasilisha hati yake.
Kipindi cha maswali na majibu:

Swali la kwanza linaelekezwa katika Wizara ya nchi, Ofisi ya serikali, Uhusiano na Uratibu.. Swali linahusu masuala ya uwekezaji. Majibu yanatolewa kwa ufupi na kueleweka.

Swali la pili sasa linaelekezwa kwa ofisi ya Waziri mkuu, TAMISEMI, Kuhusu ni vipi serikali imejipanga katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami mpaka kufikia mwaka 2015. Swali hili limeulizwa kwa niaba ya Mbunge wa Arumeru.

Swali linalofuata ni kwa Wizara ya fedha, ambalo linaulizwa na Mbunge Agustino Lyatonga Mrema, Kuhusu kwanini mishahara ya watumishi wa serikali inachelewa wakati tayari Wizara imeshatengewa bajeti? Swali linajibiwa na Naibu spika wa Bunge, Mhe. Mwigulu Nchemba, anatoa ufafanuzi.

Mbunge wa Rombo, Mhe. Selasini anauliza swali la nyongeza kuhusu ni hatua zipi zitachukuliwa kwa watumishi walioshiriki katika kupitisha malipo ya mishahara hewa?

Mwigulu anajibu na kusema hatua ya kwanza ni kusimamisha malipo hayo, na la pili ni kuwawajibisha watumishi hao ikiwa itabainika ilifanywa kwa makusudi. Anaendelea kutoa Ufafanuzi.

Mbunge wa viti maalum wa singida, Diana Chilolo, anauliza swali la nyongeza: Kwanini fedha zilizokombolewa zisitumike kulipa madeni ya walimu?

Mhe.Mwigulu anasema umeandaliwa mfumo maalum wa malipo ambao utaepusha mlolongo wa malimbikizo ya madeni ya Walimu pamoja na watumishi wengine wa serikali ili kuepusha usumbufu.

Sasa ni Maswali kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa:

Swali la kwanza limeulizwa kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Somalia na Kenya kuhusu kudai Kisiwa cha Pemba, Mhe. Bernard Membe anajibu kuwa hajapokea taarifa rasmi kutoka katika serikali hizo, ila amewataka Watanzania kuondoa hofu kuhusu hilo kwani Kisiwa cha Pemba ni mali ya Tanzania.

Swali kutoka kwa Mb. Khalifa Khalifa, anauliza kuhusu wavuvi wavamizi wanaokuja kuvua ndani ya mipaka ya Tanzania, je serikali imejipanga kukabiliana nao vipi ili kuepusha mgogoro na uhusiano mbaya na nchi wanazotoka wavuvi hao?

Mhe. Membe anajibu kuwa serikali italishughulikia hilo.

Swali lingine linaulizwa kuhusu kesi za kimataifa katika mahakama ya ICC, Nini mtazamo wa nchi za Afrika kuhusu kushitakiwa kwa viongozi wakuu wa nchi?

Anajibu kuwa nchi za Afrika zimesikitishwa na hilo kwani inajenga taswira kuwa nchi za afrika hazina uwezo wa kushughulikia masuala yake, jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni aina nyingine ya changamoto ya Afrika na nchi za Magharibi kama ilivyokuwa ubaguzi wa rangi na kadhalika.

Na amesema Kutokana na hilo, zipo baadhi ya nchi za Afrika zimetishia kujitoa katika uanachama wa ICC.

Na Katika kujibu swali la nyongeza kuhusu ni vipi serikali ya Tanzania itaepuka kushitakiwa kwenye mahakama hiyo,
Mhe. Membe amejibu kamwe serikali ya Tanzania haiwezi kushitakiwa kwa kuwa viongozi wake wanafanya kazi nzuri.

Ni zamu ya maswali kwa Wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi:

Kwa niaba ya Waziri, Mhe. Simbachawene anatoa majibu, ambapo swali liliulizwa ni lini mgogoro baina ya wakulima na wafugaji utafikia kikomo?

Jibu: Wizara imetambua kwamba ugomvi unasababishwa na uhaba wa ardhi kulingana na mahitaji na ongezeko la watu na mifugo, ndio kimekuwa chanzo kikuu cha mgogoro huo, Hivyo basi Wizara itahakikisha serikali inaanza utaratibu wa Kupima ardhi na kutoa mpango wa matumizi bora ya ardhi. Anaendelea kutoa maelezo...

Maswali kwa wizara hii bado yanaendelea..........

Wizara ya Kazi Na Ajira:

Swali linaulizwa kuhusu Ukosefu wa Ajira kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu, Je serikali inawasaidia vipi vijana kupata mikopo ili waweze kujiajiri? Na kwanini vyeti vyao visitumike kama dhamana ya kupatia Mikopo kwa kuwa hawana cha kuweka rehani katika taasisi zinazokopesha?

Mhe Gaudencia Kabaka, Anatoa ufafanuzi kuwa bado serikali haijafikiria kutunga sera hiyo, na anaeleza kuwa kazi ya serikali ni kuandaa mazingira ya wananchi wake kupata huduma kwa urahisi.

Swali la nyongeza, Mb. Viti Maalum anauliza: Je, kwanini elimu ya ujasiriamali isipewe kipaumbele ili angalau vijana na wananchi waweze kupata uwezo wa kuanzisha hata biashara zisizo rasmi ili kupunguza tatizo la Ajira?

Mhe Waziri anajibu kuwa ni wazo zuri na anasema ni jambo ambalo zipo taasisi za elimu kama VETA linatoa ujuzi mbalimbali ambazo zinawawezesha vijana kuweza kuzitumia kujiajiri.

Swali lingine ni kutoka kwa Mhe. Msabaha, anahoji kwanini serikali isiweze kuvitambua vipaji na kuviendeleza ili viweze kuwakwamua vijana kujiajiri?

Jibu linatolewa kuwa, Serikali inavitambua vipaji na ipo kwenye mchakato wa kuviwezesha ili vitoe ajira kwa VIjana ambao wataweza kuajiri na wengine.

Sasa ni Wizara ya Maliasili na Utalii:

Kuhusu vipuri vilivyokamatwa, je ni hasara kiasi gani serikali imepata na imejipanga vipi kuzuia tatizo la ujangiri lisiendelee?

Jibu kwa niaba ya Waziri: Hasara za kiuchumi ni takribani, Bilion 3, 4, 680 000, Na mpk sasa serikali imewakamata majangiri 556 na kesi zao zinaendelea, na bado Wizara inachukua hatua mbalimbali za kupambana na Ujangiri, kama vile kuhifadhi na kuimarisha ulinzi, kutoa mafunzo zaidi kwa watumishi na kuwapatia vifaa vya kutosha vya kutendea kazi.

Swali la nyongeza: Je, Wizara imejipanga vipi kushughulikia hizo kesi za Majangiri ili Wananchi waweze kuridhika na hatua watakazochukuliwa hawa waporaji wa mali za umma?

Anajibu: Kesi zitashughulikiwa haraka iwezekanavyo.

Mhe. Anna kilango Malecela anauliza swali la nyongeza: Kama Serikali inapambana na Ujangiri, kwanini inatoa vibali vya Uwindaji?

JIbu: Hili ni suala la kimkataba, kwahiyo kama lina haja ya kujadiliwa, basi serikali itabidi ilitazame upya.

Swali: Sekta ya utalii ni moja ya chanzo kikubwa na cha kasi cha mapato, Je serikali imejipanga vipi kudhibiti swala la athari za utamaduni?

Jibu: Kukua na kuingiliana kwa utandawazi kunapelekea mwingiliano wa watu na jamii tofauti, hivyo swala la kuathiriwa kwa tamaduni ni changamoto kubwa, hata hivyo serikali imeweka mikataba itakayowawezesha wageni kuheshimu mila na tamaduni za nchi. Na pia kuna mpango wa serikali wa kuweza kuzuia matumizi ya teknolojia kulingana na umri. Pia Kuhusu mavazi, serikali itatia mkazo suala la vazi la taifa.

Swali la Nyongeza, linahusu mavazi yasiyo ya kistaarabu pamoja na tabia ambazo zipo kinyume na tamaduni, Je serikali inashughulikia vipi tabia hizi zinazoshamiri kwa kasi katika jamiii?

JIbu: Malezi ni wajibu wa serikali na wazazi, kwahivyo kila upande uwajibike ipasavyo.

Wizara ya Nishati na Madini:

Swali likiulizwa na Mb. Freeman Mbowe, kuhusu mpango wa serikali kusambaza umeme vijijini, Hususani kwa Wilaya ya HAI mkoani Kilimanjaro.

Naibu Waziri Charles Kitwana anajibu kuwa serikali kupitia wizara ya nishati inatarajia kuanza kusambaza umeme vijijini kupitia mradi wa REA, na utekelezaji umefikia 26%.

Mhe. Joseph Selasini anauliza swali la nyongeza: Miundombinu ya umeme Wilaya ya Hai imechakaa sana kiasi cha kupelekea madhara kwa wananchi hadi vifo, Je serikali itachukua hatua gani ili kutatua uchakavu wa miundombinu?

Jibu: Ni kweli, kutokana na baadhi ya miundo mbinu kuwa ni ya muda mrefu ndio maana inachakaa, ila serikali kupitia Tanesco itaanza mchakato wa kupitisha njia mpya za umeme kuanzia Dar es salaam hadi Segera, kisha nyingine kuanzia Tanga na kuendelea huko vijijini kote. Mpango huo upo na utafanywa haraka.

Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika:

Swali: Kuna haja ya wakulima kuendelea kuzalisha mazao ambayo hawana manufaa nayo baada ya kusainishwa vocha ambazo zilijaa udanganyifu?

Jibu: Serikali inasikitishwa na udanganyifu ambao umefanyika kwa wakulima kwa hizo vocha ambazo zimewanyima fursa ya kupata hata pembejeo bora kwa ajili ya uzalishaji. Na nia ya serikali ilikua ni nzuri katika hili jambo. Hata hivyo, serikali inawashikilia baadhi ya mawakala na itawachukulia hatua kali za kisheria. Pia Wameisababishia hasara kubwa serikali.

Nyongeza: Kwanini serikali isitoe ruzuku moja kwa moja kwa wakulima?

Jibu: Serikali itafanya mpango wa namna ruzuku zitakavyoweza kuwafikia wakulima kupitia utaratibu maalum utakaoanzishwa. Kwa sasa Serikali Imeanza na utaratibu wa kutoa ruzuku kupitia taasisi za fedha kwa mfano CRDB, NMB na benki nyinginezo zimeanza kutoa huduma hiyo.

Muda wa Maswali na Majibu Umeisha...

============================== ============================== ===============

UPDATE:

Kikao cha Bunge kimehairishwa mpaka saa kumi Jioni na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Job Ndugai.

No comments:

Post a Comment