JESHI la Anga la Marekani limetangaza kuwa limefanyia
majaribio kombora la Balestiki linaloweza kuvuka mabara na kwamba majaribio
hayo ni ujumbe kwa walimwengu kuhusu uwezo wa silaha za nyuklia wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Anga la
Marekani, kombora la Minuteman-III lilifanyiwa majaribio mapema Jumatatu katika
kituo cha Jeshi la Anga cha Vandenberg huko California. Taarifa ya Jeshi la
Anga la Marekani imesema: Majaribio hayo ya kombola la balestiki la nyuklia
yanaonesha picha ya wazi kwa walimwengu kuhusu uwezo wa kombora ya
Minuteman-III ambalo linaweza kulenga mahala popote.
Kombora la Balestiki linavyolipuka.
Kwa kutilia maanani kwamba Jeshi la Anga la Marekani
haliwezi kutumia makombora ya Peace Keeper kwa mujibu wa makubaliano ya silaha
ya START II (Strategic Arms Reduction Treaty),
kombora la Minuteman-III litakuwa kombora pekee la balestiki
linaloweza kuvuka mabara la jeshi la Marekani. Kombora hilo linavishwa kichwa
cha silaha ya nyuklia aina ya W87 ambacho kina uwezo mkubwa wa uharibifu.
Majaribio hayo yamefanyika sambamba na mazoezi ya kijeshi yanayoendelea
kufanywa na majeshi ya shirika la NATO huko Ulaya mashariki.
Inaonekana kuwa kwa majaribio ya kombora hilo la nyuklia,
jeshi la Anga la Marekani linafuatilia malengo kadhaa.
Kwanza ni kuwa Marekani inataka kuonesha misuli na uwezo
wake wa silaha za nyuklia kwa wapinzani wake wakubwa hususan Russia. Katika
kipindi cha miaka kama miwili iliyopita jeshi la Russia limefanya majaribio
mtawalia ya makombora yanayoweza kuvuka mabara (Intercontinental Ballistic
Missile au IBM) na hata kurusha makombora kama hayo kwa kutumia nyambizi. Kwa
msingi huo Marekani ilikuwa ikinyemelea fursa ya kukabiliana na majaribio hayo
ya silaha za nyuklia ya Russia.
Suala la pili ni kushadidi mivutano baina ya Russia na NATO
huko Ulaya Mashariki ambako kumezifanya pande hizi mbili zijizatiti kwa silaha
na majeshi katika eneo hilo na katika Bahari Nyeusi. Kwa msingi huo Marekani
inataka kumuonesha adui wake yaani Russia, kwamba iwapo mgogoro huo utaendelea
inaweza kutumia silaha zake za nyuklia.
Marekani ni miongoni mwa wamiliki wakubwa zaidi wa silaha za
nyuklia duniani na ndiyo nchi pekee ambayo hadi sasa imetumia silaha hizo kuua
watu wa taifa jingine. Nchi hiyo kinyume na ahadi zake za kupunguza maghala
yake ya silaha za nyuklia, ingali inastawisha na kupanua zaidi silaha hizo na
kuzifanyia majaribio.
Marekani pia inasasisha na kuziboresha zaidi silaha zake za
zamani za nyuklia licha ya harakati za kimataifa za kupunguza silaha hizo
husuan mkataba wa NPT unaosisitiza kupunguzwa na hatimaye kuangamizwa kabisa
silaha hizo. Katika uwanja huo Washington imetenga bajeti ya dola bilioni 355
ambazo zitatumika kusasisha na kuboresha mitambo yake ya silaha na kuinua juu
kiwango cha majaribio ya silaha za nyuklia. Vilevile Marekani imechukua hatua
za kuboresha silaha na maghala yake ya zana za nyuklia barani Ulaya yakiwemo
mabomu ya nyuklia ya B-61.
Kwa utaratibu huo, Washington, kinyume na mikataba ya
kimataifa ya kuzuia uzalishaji wa silaha za nyuklia, inaendelea kuzalisha na
kufanyia majaribio silaha za aina hiyo, suala ambalo linakiuka mkataba wa NPT.
CHANZO: IRAN SWAHILI



No comments:
Post a Comment