Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, November 4, 2015

UFAFANUZI WA TUKIO LA KUANGUKA KWA JUKWAA LA JENGO LA NHFI MKOANI MBEYA.

nh1
Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti akifafanua jambo wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusu kuvunjika kwa uzio wa jengo la mfuko huo linalojengwa mkoani Mbeya kutokana na kukumbwa na mvua na upepo mkali, amesema jengo hilo liko salama kabisa ila uzio unaosaidia kuwakinga wajenzi ndiyo ulioanguka kutokana na upepo huokulia ni Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF,Bw Rehani Athuman.
nh2
Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti akifafanua jambo wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusu kuvunjika kwa uzio wa jengo la mfuko huo linalojengwa mkoani Mbeya.
nh3
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF,Bw Rehani Athuman akionyesha mchoro wa jengo hilo kwa waandishi wa habari, kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti
 
......................................................................................................
Utangulizi:
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hivi sasa unaendelea na ujenzi wa majengo katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kujitosheleza kwa majengo ya ofisi na kukidhi mahitaji ya wanachama wake na wadau wengine.
Moja ya mikoa ambayo inaendelea na ujenzi huo ni Mbeya, ambako Mfuko unajenga jengo la ghorofa kumi na mbili litakalokuwa na nafasi za ofisi na huduma nyingine ndani yake.
Tukio la Kuanguka kwa jukwaa:
Wakati shughuli hizo za ujenzi zinaendelea, jana mchana katika hali isiyotarajiwa mvua iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha mjini Mbeya. Upepo na mvua hizo vilisababisha kuanguka kwa jukwaa la jengo hilo na kutua juu la paa la jengo la ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Mbeya. Kuanguka kwa jukwaa hilo hakukuwa na madhara yoyote kwa maisha ya binadamu, kwa maana kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha au kupata majeraha. Hata hivyo tukio hilo lilisababisha taharuki kwa wafanyakazi wapatao hamsini waliokuwemo ndani ya jengo hilo na hivyo kusababisha kazi kusimama kwa muda. Aidha tathmini ya awali iliyofanyika katika paa la jengo la TANESCO lililoangukiwa na jukwaa hilo inaonyesha kuwa paa hilo ilipata hitilafu ndogo ambayo itafanyiwa marekebisho kwa gharama za Mkandarasi anayejenga jengo la NHIF.
Hatua za kisualama zilizochukuliwa:
Kama sheria za ujenzi zinavyoagiza, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo hilo Mkandarasi alishajenga uzio kuzunguka jengo zima ili kuhakikisha kuwa shughuli za ujenzi hazileti madhara kwa wapita njia au ofisi zilizo jirani. Umakini wa Mkandarasi huyo katika kuzingatia taratibu za tahadhari katika shughuli za ujenzi, umewezesha jengo hilo la ghorofa kumi na mbili kufikia hatua nzuri ya ujenzi bila madhara yoyote kwa wajenzi wenyewe, wapita njia au ofisi za jirani.
Aidha kufuatia tukio la Jumatatu 02/11/2015, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeshamwandikia Mkandarasi anayeendelea na ujenzi katika jengo hilo kuhakikisha kuwa uzio unaozunguka jengo zima unaimarishwa zaidi hususani wakati huu tunapokaribia kipindi cha mvua za masika ili kuepuka uwezekano wa madhara yoyote kwa binadamu wakati shughuli za ujenzi zinaendelea.
Namna Habari ilivyoripotiwa:
Tunapenda kuufahamisha umma kwamba habari zilizoripotiwa jana na baadhi ya vyombo vya habari kwamba jengo la NHIF mkoani Mbeya limeporomoka, zilipotosha ukweli wa tukio hilo, kwani kilichoporomoka siyo jengo, bali ni jukwaa.
Tunapenda kusisitiza kuwa tukio hilo limesabishwa na mvua kubwa na upepo uliovuma katika mji wa Mbeya, wala siyo uzembe wa Mkandarasi anayejenga jengo hilo.
Wito kwa Wanachama wa NHIF:
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unawaomba wanachama na wadau wake nchini kote waendelee kuwa watulivu na kuvuta subira kwani changamoto ya ufinyu wa ofisi katika mikoa itakuwa imepatwa ufumbuzi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya unaoendelea hivi sasa katika mikoa mbali mbali nchini.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

No comments:

Post a Comment