Uongozi
wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umetangaza kuhamishia mjini Dodoma huduma zake
za usafirishaji kuanzia Ijumaa ya wiki
hii Januari 29, 2016.
Taarifa
hiyo imebainisha kuwa huduma hizo
zinahamishiwa kwa muda mjini Dodoma hadi pale kazi ya ukarabati ya tuta la reli
litakapo tengemaa kati ya Stesheni za Kidete na Kilosa mkoani Morogoro.
Halikadhalika
kutokana na mafuriko ya eneo hilo kutojulikana lini yataisha, Uongozi umeamua kwa
sasa kusitisha zoezi la ukarabati ili kuokoa rasilimali zinazotumika katika ukarabati
wa eneo hilo. Hata hivyo kazi ya kuzuia uharibifu zaidi dhidi ya tuta la reli
inaendelea kulingana na hali inavyojitokeza.
Wakati huo huo Uongozi wa TRL umeandaa
utaratibu na Wamiliki wa mabasi kuwasafirisha abiria wake watakaotumia huduma
zake zinazoanzia siku za Jumanne na Ijumaa mjini Dodoma kutokea Dar es Salaam.
Sehemu ya uta la reli kati ya Stesheni za Kidete na Kilosa mkoani Morogoro ambalo limesombwa na mafuriko ya maji.
Mafundi wakielekea sehemu ya tatizo kwa kutumia viberenge
Taarifa
imefafanua kuwa wakati maombi ya huduma za kusafirisha shehena yataanza
kupokelewa Ijumaa Januari 29, 2016 hata hivyo treni ya kwanza ya abiria imepangwa kuondoka
saa 2 usiku siku ya Jumanne Februari 2,
2016 Dodoma..
Kwa
taarifa hii TRL inawatangazia wananchi kwa ujumla kuwa wanaweza kuanza kukata
tiketi za safari ya Jumanne wakati wowote mara baada kusoma taarifa hii katika
stesheni za reli ya kati zilizo
karibu yao.
Uzoefu
unaonesha katika miaka ya 1998 na 2010 huduma za reli zilihamishiwa Dodoma kwa
muda baada ya eneo kati ya Gulwe, Godegode mkoani Dodoma , Kidete na Kilosa mkoani Morogoro kukumbwa na mafuriko makubwa na
kuisambaratisha njia ya reli kabisa katika maeneo hayo.
Taarifa
imefafanua kuwa japo hatua hiyo itaongeza gharama lakini ni muhimu kwa huduma
za usafirishaji ziendelee ili kusaidia Watanzania kichumi na kijamii kadri inavyowezekana.
Imefahamika kuwepo huduma ya reli kunapunguza kasi ya uharibifu wa barabara
zetu ambazo sio muda mrefu zimejengwa kwa gharama kubwa kutokana na fedha za
walipa kodi wa Tanzania.
Imetolewa
na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Elias Mshana.
Dar
es Salaam,Chanzo Issa Michuzi
No comments:
Post a Comment