Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, March 10, 2016

WAFANYABIASHARA WAIGOMEA SERIKALI KUSHUSHA BEI YA SUKARI

Licha ya Bodi ya Sukari Tanzania kutangaza bei elekezi ya bidhaa hiyo kuwa ni Sh1,800 kwa Dar es Salaam, maeneo mbalimbali jijini inauzwa kwa Sh2,200.

Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Henry Semwanza alisema bei hiyo itatumika kwa maduka yote ya rejareja na wafanyabiashara wanatakiwa kuizingatia pamoja na kuendelea kusambaza sukari kwa wingi.

Waandishi wetu waliotembelea maeneo mbalimbali yakiwamo Manzese, Magomeni, Kariakoo, Kisutu na Gongo la Mboto walibaini kuwa mfuko wa sukari wa kilo 50 ulikuwa unauzwa Sh97,000 hadi Sh100,000 huku wa kilo 25 ukiuzwa kuanzia Sh48,000 hadi Sh50,000.


Mfanyabiashara wa duka la jumla eneo la Manzese, Alex Brayton alisema alikuwa akiuza sukari kwa bei ya rejareja Sh2,200 na kwamba sababu kubwa ni kwamba sukari inayozalishwa viwandani haionekani wala haitoshelezi hivyo wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wanawauzia kwa bei ya juu.

“Suala la kushusha sukari hadi kufikia Sh1,800 kwa bei elekezi halitawezekana kwa kuwa bei ya jumla ya kilo moja tunauziwa Sh2,000 hivyo tunalazimika kuuza Sh2,200 ili kilo moja tupate faida ya Sh200,” alisema Brayton. Mfanyabiashara mwingine wa duka la jumla Magomeni, Idrisa Abraham aliyekuwa akiuza mfuko wa sukari wa kilo 50 kwa Sh98,000 na wa kilo 25 kwa Sh48,000, alisema kabla ya kutoa bei elekezi, Serikali ilitakiwa kufanya utafiti ili kubaini sababu ya kutoonekana kwa bidhaa hiyo na kukutana na wafanyabiashara wanaosambaza na wa maduka ya jumla ili kujua kwa nini sukari ya Tanzania haionekani na kinachoifanya kupanda “...nina imani wangebaini kitu, kinachonishangaza sukari iliyokuwa inatoka Malawi na Brazil ilikuwa inauzwa kwa bei nafuu sana na ilikuwa inalipiwa kodi kwa nini ya Tanzania iwe bei juu?”

Mfanyabiashara wa duka la rejareja eneo la Gongo la Mboto, Issa Salmin alisema wanauziwa kwa bei ya jumla Sh2,000 hivyo wanalazimika kuuza kwa Sh2,200.

Mfanyabiashara wa rejareja Ubungo – Msewe, Joseph Masawe alisema siyo rahisi kushusha bei ghafla wakati wafanyabiashara wakubwa waliwauzia kwa bei ya juu.

Alisema wataweza kufanya hivyo ikiwa wafanyabiashara wakubwa watashusha bei na ile waliyokwishanunua na kuihifadhi kwenye maghala itakuwa imemalizika.

Masawe alisema Serikali inatakiwa kutengeneza mfumo utakaowabana wafanyabiashara wakubwa ambao ndiyo chanzo cha kupanda kwa bei ya sukari.

“Huwezi kutwambia tushushe bei ya bidhaa zilizo sokoni wakati tulinunua kwa bei kubwa, cha msingi Serikali iwadhibiti wafanyabiashara wakubwa ili washushe bei, vinginevyo itaendelea kuwa kama maigizo,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine wa Mabibo, Henry Mwinuka alisema anauza sukari kwa Sh2,200 baada ya kununua mfuko mmoja kwa Sh90,000 bei ambayo ilikuwa juu.

“Nilinunua mifuko 15, kila mmoja Sh90,000. Ikiwa nitashusha bei itakuwa hasara kubwa kwangu, lazima iishe kwanza ndipo tushushe na tutafanikiwa ikiwa bei iliyo sokoni itakuwa chini ya Sh80,000,” alisema.

Alisema iwapo Serikali inataka kudhibiti bei ya bidhaa hiyo, lazima iwabane wafanyabiashara wakubwa ambao wamekuwa wakijinufaisha kwa kuingiza sukari ya magendo na kukwepa kodi.

“Kuna sukari inayoitwa KK ‘Grade four’ inasambazwa kama kawaida wakati haitakiwi hata kidogo kutokana na kiwango chake.

Serikali haijaweza kabisa kuidhibiti. Hili ni tatizo,” alisema.

Pia, alisema kuna janja imeanza kutumika kwa kuhifadhi sukari hiyo kwenye mifuko ya kampuni za viwanda vya ndani, jambo ambalo ni hatari zaidi.

No comments:

Post a Comment