Utata
umegubika mauaji ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow,
baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi usiku wa
kuamkia jana.
Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, aliwaambia waandishi wa habari ofisini
kwake jana kuwa Barlow, aliuawa maeneo ya Kitangiri katika barabara
inayoelekea Bwiru, jirani na hoteli ya Tai Five jijini hapa. Alisema
mauaji hayo yalifanyika kati ya saa 7 na saa 8 usiku, wakati Barlow
akimsindikiza mwanamke aliyejulikana kama Doroth Moses. Inasemekana kuwa
wote wawili, walikuwa wametoka kuhudhuria kikao cha maandalizi ya
harusi ya mtoto wa dada wa Barlow, kilichofanyika hoteli ya Florida.
Hata
hivyo, taarifa zisizo rasmi kutoka mitandao ya kijamii kuhusu utata wa
mauaji hayo, zinaeleza kuwa Barlow na mwanamke huyo walikuwa wanatoka
katika hoteli inayotajwa kwa jina la La-Kairo. Akifafanua, Ndikilo
alisema Barlow alikuwa akiendesha gari yake binafsi aina ya Toyota
Hilux- double cabin na kwamba alikuwa akimsindikiza mwanamke huyo kwenda
nyumbani kwake.
Mwanamke
huyo ambaye anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi, ni mwalimu
katika Shule ya Msingi Nyamagana. Alisema wakati wakikaribia eneo la
Kitangiri anakoishi mwanamke huyo, waliwaona watu wawili wakiwa wamevaa
mavazi maalum (jackets) yanayovaliwa na wananchi wanaoshiriki ulinzi
shirikishi unaofahamika pia kama polisi jamii. Kwa mujibu wa Ndikilo,
baada ya kuwaona watu hao ambao waliwamulika kwa tochi, Doroth
alimuuliza Barlow iwapo anawafahamu, naye alimjibu kuwa watakuwa ni
polisi jamii.
Hata
hivyo, Ndikilo alisema baada ya Barlow kusimamisha gari pembeni, mkabala
na nyumba anayoishi mwanamke huyo, watu hao wawili waliwasogelea huku
wakionyesha kukerwa na mwanga wa taa za gari. Alisema watu hao walimhoji
Barlow kwa nini anawamulika kwa taa za gari, lakini wakati akijaribu
kutoa ufafanuzi kwamba yeye ni RPC, ghafla walitokea watu wengine
wapatao watatu, walisimama kuzunguka gari la Kamanda huyo.
Baada ya
kuona hali hiyo, huku akijaribu kuwauliza iwapo hawamfahamu kuwa yeye
ndiye RPC na kutoa radio call (simu ya upepo) ili kufanya mawasiliano na
polisi wa doria. “Ghafla mmoja wa watu hao alitoa bastola na
kumfyatulia risasi ambayo iliingilia shingoni na kutokea upande wa pili
wa bega,” alisema Ndikilo.
Alisema
baada ya tukio hilo, watu hao walichukua vitu kadhaa ikiwemo bastola,
simu na radio call alivyokuwa navyo Barlow na kutoweka kusikojulikana.
“Kimsingi mazingira ya mauaji yenyewe bado yana utata, lakini Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya mkoa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tunafanya
kazi ya kuchunguza ili kuujua ukweli,”alisema.
Kwa
mujibu wa Ndikilo, baada ya kufyatuliwa risasi inaaminika Barlow alikufa
papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi na mwili wake umehifadhiwa
katika hospitali ya rufaa ya Bugando ukisubiri taratibu za mazishi.
Alisema kutokana na mazingira hayo ya utata ya mauaji, Jeshi la Polisi
linamshikilia mwanamke aliyekuwa naye kwa mahoajiano zaidi. Taarifa za
awali zilidai kwamba mwanamke huyo anayesadikiwa kuwa ni mjane, ni dada
yake Barlow.
Lakini
baadaye jana, Mkuu wa mkoa wa Mwanza alikanusha taarifa hizo na
kusisitiza kuwa ni mtu ambaye alikuwa amempa lifti wakati wakitoka
katika kikao cha harusi. Kufuatia mauaji hayo Ndikilo alisema kuwa
Polisi Makao Makuu, limemtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI) Robert Manumba kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio hilo.
Nyumbani
kwa Doroth, kijana Kenrogers Edwin aliyejitambulisha kama mtoto wa kaka
yake wa mwanamke huyo, alisema kabla ya tukio hilo, shangazi yake
(Doroth) alipiga simu ili wamfungulie geti. Alisema kwamba wakati
akifungua geti, aliona gari likiwa limeegesha huku watu wawili wakiwa
upande wa abiria na wengine watatu wakiwa upande wa dereva na kisha
alisikia mlio wa risasi na baadaye watu hao walitimua mbio baada ya
kuona pikipiki inakuja nyuma yao.
Baadhi ya
wananchi waliozungumzia mauaji hayo walielezea kushangazwa kwao na
hatua ya Barlow kutembea usiku bila mlinzi wake (bodyguard) ambaye kwa
kiwango kikubwa angeweza kusaidia kumuepusha na kifo.
IGP MWEMA AMTUMA DCI KWA UPEPELEZI
Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, katika taarifa aliyoitoa jana
jijini Dar es Salaam, alisema ameshamtuma Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai DCI Robert Manumba, mkoani humo kuimarisha ulinzi na
upepelezi wa tukio hilo.
Aidha,
Mwema amewaomba wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa jeshi
hilo, utakaowezesha kuwabaini wahalifu hao. Akielezea kuhusu mauaji
hayo, Mwema alisema, wakati huo Barlow alikuwa akitokea kwenye kikao cha
harusi ya ndugu yake eneo la Florida hoteli Mwanza mjini. Alisema
alikuwa ameongozana na ndugu yake wakitoka kwenye kikao hicho. Alisema
tukio hilo limewashtua na kuwahuzunisha na kwamba wakati uchunguzi
ukiendelea, wataendelea kutoa taarifa kadri wanakavyozipata. ….
MAKAMANDA WA MIKOA WATOA KILIO
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali
nchini, wamesema kuwa wamempoteza kiongozi mwenye uzoefu wa muda mrefu
kazini na aliyekuwa mchapakazi katika jeshi hilo. Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema ukomavu wa kazi ndio
uliosababisha kamanda huyo kupelekwa katika mkoa ambao ni miongoni mwa
mikoa migumu nchini.
Alisema
enzi za uhai wake, alikuwa akiwaelimisha wenzake ili waweze kufanya kazi
kwa ufanisi na kwamba alikuwa mwepesi kuwarekebisha wale wanaoenda
kinyume na kazi. Kenyela alisema kwa upande wake atamkumbuka kwa sababu
ndiye aliyempokea wakati akianza kazi hiyo na alikuwa akiishi naye
kwenye kambi za maofisa huko Tabata.
“Wito
wangu kwa wananchi walaani vitendo vya mauaji ya viongozi kwa sababu
kumpoteza kiongozi ni gharama kubwa katika nchi hasa ukiangalia muda
uliotumika kumuandaa hadi amefikia hatua hii,” alisema. MOROGORO Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema kuwa, ameguswa
na msiba huo wa ghafla na kueleza kuwa, atamkumbuka daima kwa kuwa
alikuwa akifanya kazi yake kwa kujiamini.
“Tumempoteza
jembe kwa sababu alikuwa mzoefu kwenye kazi na asiye mchoyo pindi
umwombapo ushauri, kwa wale wachanga kwenye kazi walikuwa wakimtumia
sana ili waweze kuifanya kazi yao kwa ufanisi,” alisema. MTWARA Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki amewataka wenzake, kuyaenzi na
kuyaendeleza yale mazuri aliyokuwa akiyafanya Barlow enzi za uhai wake.
TANGA
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, ameeleza kusitikitishwa na
mauaji ya Barlow na kuwataka watumishi wa jeshi hilo kuwa wavumilivu
wakati wakisubiri uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea ili hatua madhubuti
ziweze kuchukuliwa.
“Kwa
sababu kuna kikosi maalum ambacho kimeenda kufanya uchunguzi wa mauaji
hayo basi nawasihi wenzangu tuendelee kuwa wavumilivu mpaka hapo
upelelezi utakapokamilika na kujua hatma yake au hatua gani za kuchukua,
“alisema. Alimwelezea marehemu alikuwa mtu mchapa kazi, mvumilivu na
aliyeipenda kazi yake na kwamba ameacha pengo kubwa katika nafasi hiyo.
KILIMANJARO Kamanda
wa Polisi mkoani Kilimanjaro Robert Boaz, amesema kifo cha Barlow ni
cha kawaida ambacho kinaweza kumkuta mtu yeyote na haipaswi kujiuliza
maswali mengi. Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Boaz alisema
kifo hicho kinaweza kikamkuta hata rais wa nchi yoyote ambaye analindwa
na walinzi chungu nzima.
“Kifo
chake kinatupa majonzi sisi makamanda wenzake,lakini kikubwa kilichobaki
ni kumuombea kwa Mungu na kuacha uchunguzi kufanyika,” alisema.
Aliongeza, “kwa sasa ni mapema mno kuzungumza chochote,lakini
ninachoweza kusema ni kuwa kifo chake kimenistua na ni kifo ambacho
kinaweza kikamtokea mtu yeyote.”
Aidha kwa
upande wao baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro wameeleza kushangazwa
na kiongozi mkubwa wa Polisi kuuawa na majambazi. Bariki Sanga mkazi wa
Kilimanjaro aliliambia NIPASHE Jumapili kuwa,ni jambo la kujifunza kwa
kila kiongozi na kila raia kuwa mlinzi wa mali zake mwenyewe.
MBEYA
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, amesema amepokea kwa mshtuko na
masikitiko kifo hicho. Alisema ingawa hapaswi kulitolea tamko kwa kuwa
linashugulikiwa na Polisi Makao Makuu, kifo hicho ni changamoto kubwa
kwa jeshi hilo ambalo sasa linatakiwa kujipanga na kufanya kazi kwa
bidii. Alisema kuwa yeye binafsi anamfahamu vizuri Barlow kwa kuwa
alimpokea vizuri wakati yeye (Diwani) alipoteuliwa kwa mara ya kwanza
kuwa Kamanda wa Polisi wa mkoani Shinyanga.
Alisema
Barlow pia alikuwa ni mwenyekiti wa Makamanda wa Polisi wa Kanda ya Ziwa
ambaye alikuwa akiwaunganisha vizuri na kupunguza kabisa matukio ya
uhalifu kwenye kanda hiyo. Aliongeza kuwa kwa vyovyote ambavyo uchunguzi
utakavyobaini, kifo cha Barlow ni pigo kwa Polisi, kwa kuwa mchano wake
ulikuwa bado unahitajika sana ndani ya jeshi hilo.
DODOMA
Kamanda
wa Polisi Mkoani Dodoma, Stephen Zelothe, ambaye Barlow alikuwa
mwanafunzi wake kikazi, alisema ni masikitiko makubwa kutokea kwa tukio
hilo. “Ni masikitiko makubwa kutokea kwa jambo hili…siwezi kusema lolote
tuache kwanza mambo ya kidunia (mazishi) yapite,”alisema Zelothe kwa
masikitiko makubwa alipoulizwa nini kifanyike
No comments:
Post a Comment