SALAAM,
JANA na leo, zimetolewa habari tofauti
kuhusiana na kalbu ya Simba ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee
ufafanuzi kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa
taarifa hizo.
1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina
ya Simba na Coastal Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel
alitoa taarifa kwa uongozi wa Simba kwamba ataizuia timu isiondoke
hotelini kwa vile anaidai Sh milioni 25 na anataka alipwe zote jana.
Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa
hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na wachezaji wote wa
Simba katika hoteli hiyo usiku wa kuamkia jana.
Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa
taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki
hao hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi na walisubiri mpaka wakati timu
inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua hiyo.
Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa
ya ghafla mno. Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba
ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika
kipindi cha miezi 10 iliyopita.
Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya
Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni
kwamba klabu yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu
wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.
Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya
kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai
zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai zaidi
ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na
Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha hizo.
Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba
itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi
na makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya
kimaendeleo.
Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake
inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa kadri
itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya klabu
ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya KILIMANJARO
ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na
matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini
kokote walipo duniani ili kuongeza mapato yake. Tayari mawasiliano
yameanza na wenzetu wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest
in Africa ili Simba nayo ifaidike.
Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe
kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa na tajiri
duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina
madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu
ingeweza kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati)
yaonekane kama kitu kigeni?
Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni
yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit
worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba
inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima
kubwa na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya
nchi.
No comments:
Post a Comment