WAKATI
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa
Ponda, akiendelea kuuguza jeraha linalodaiwa kutokana na risasi katika
mahabusu ya Segerea, jijini Dar es Salaam, wingu jingine la mashaka
limeizunguka familia yake. Mashaka hayo yanatokana na kitendo cha
makachero wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakiwemo wale wa Uhamiaji
kudaiwa kuvamia nyumbani kwa wazazi wake, Ujiji mkoani Kigoma, kwa nia
ya kuilazimisha familia yake wachukuliwe damu kwa ajili ya vipimo vya
vinasaba (DNA). kabla na baada ya tukio la sasa la Sheikh Ponda kupigwa
risasi, makachero hao wamejaribu kuifikia familia hiyo ya Ponda kwa
takribani mara tano bila mafanikio yoyote.
Mmoja wa wanafamilia hao ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini
akihofia usalama wake, amelidokeza kwamba makachero hao baada ya
kushindwa kuwashawishi kutoa damu, wakataka wapatiwe mate au nywele kwa
ajili ya kufanyia kipimo hicho ili kutambua kama Ponda ni ndugu yao na
pia ni raia wa Tanzania.
“Tulikwisha shawishiwa sana, wakati fulani walitukatia hadi tiketi za
ndege ili tuje Dar es Salaam kwa ajili ya kipimo hicho pamoja na
kufanya mahojiano maalumu, lakini tulikataa, kwa sababu hawa jamaa
wanaogopesha,” alisema mwanafamilia huyo.
Alisema baada ya kukataa kutoa damu, ndipo walipofika kwa mara
nyingine tena wakitaka kuchukua nywele za mama yake mzazi Ponda pamoja
na za baadhi ya ndugu zake, lakini hilo nalo likashindikana baada ya wao
kugoma.
“Tangu Sheikh Ponda aumizwe mama yake mzazi amekuwa mgonjwa, baada ya
kupokea taarifa hizo kwa mshituko, hata hivyo familia kwa ujumla haina
uhuru tena kwa sababu imekuwa ikifuatwafuatwa na makachero hao pamoja na
watu wa Uhamiaji.
“Kwa kweli hofu imetanda katika familia yetu na hatujui nini
kinafuata kutokana na kuendelea kufuatiliwa na makachero, kwa mfano ile
hatua ya kupewa tiketi ili kwenda Dar es Salaam ilitufanya tushituke kwa
hofu ya kwamba labda kuna mpango wa kudhuru maisha yetu, wamekwisha
kuja mara nyingi, wameomba mpaka kitabu wamekitoa mpaka nakala,
alichoandika Sheikh Ponda, kinaitwa ‘Tanu mkoani Kigoma mwaka 1954’,”
alisema mwanafamilia huyo.
Wakati taarifa hizo zikiibuka sasa, kwa muda mrefu sasa kumekuwapo na
habari za kukanganya juu ya asili ya Sheikh Ponda Issa Ponda, wengine
wakidai kuwa ni raia wa nchini Burundi, taifa ambalo linapakana na mkoa
wa Kigoma, sehemu inayoelezwa ndiko alikozaliwa. Hata hivyo ndugu zake
wanadai kuwa wao ni raia halali wa Tanzania
Wakati huo huo, chanzo kingine cha habari kimelidokezea gazeti hili
jinsi Sheikh Ponda alivyofanikiwa kuwakwepa polisi Zanzibar, baada ya
kudaiwa kutoa kauli za uchochezi katika mhadhara wa Kiislamu wakati
wakiwa visiwani humo.
Inadaiwa kwamba Sheikh Ponda kabla ya kuhutubia mhadhara huo alipita
gerezani kumuona kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu
Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed.
Kwamba baada ya kumaliza kuhutubia mhadhara huo, alianza safari ya
kuelekea katika msikiti wa Mbuyuni, ambako alihitajika kwa kuendesha
mhadhara mwingine.
Chanzo hicho kinasema wakati akiwa njiani alipata taarifa kwamba
Polisi wameweka mitego ya kumkamata katika maeneo mbalimbali kama
bandarini na uwanja wa ndege, hivyo akashindwa kufika katika msikiti
huo.
“Baada ya kubaini kuna mitego ipo kila sehemu, alikwenda bandarini
kwa ajili ya kupanda boti za kwenda Dar es Salaam na hapo alionekana
akiongea na watu mbalimbali, lakini baadaye alitoweka ghafla na
haikujulikana mara moja alikoelekea,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kingine cha habari kililidokeza gazeti hili kuwa Sheikh Ponda
alitoroka katika eneo hilo baada ya kubaini kwamba tayari alikuwa
anaingia kwenye mtego wa polisi.
Baada ya kutoweka ghafla, inadaiwa kuwa Sheikh Ponda alipanda
majahazi ya usiku ya kutoka visiwani humo kuelekea Bagamoyo na hivyo
akafanikiwa kukwepa mitego yote iliyokuwa imewekwa na Jeshi la Polisi
Zanzibar.
Sheikh Ponda ambaye kwa sasa yupo mahabusu katika gereza la Segerea,
anakabiliwa na mashitaka ya uchochezi sehemu mbalimbali nchini kuanzia
Juni 2 mpaka Agosti 11, mwaka huu, kwa mujibu wa shitaka alilofunguliwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mbali na shitaka hilo, pia Sheikh Ponda anadaiwa amesababisha
mkanganyiko mkubwa katika jamii, kuhusu ukweli wa jeraha analodai kwamba
linatokana na risasi aliyopigwa na polisi mkoani Morogoro Jumamosi
iliyopita.
Mkanganyiko huo unatokana na Hospitali aliyokuwa akitibiwa ya
Muhimbili, Kitengo cha MOI kushindwa kuthibitisha kama jeraha lake
limesababishwa na risasi ama la!
Pia kauli zake za uchochezi anazodaiwa kuzitoa katika mhadhara wa
Kiislamu mjini Zanzibar zinatajwa kuwa nyuma ya tukio la kumwagiwa
tindikali raia wawili wa Uingereza, japokuwa yeye tayari amekanusha kwa
vyombo vya habari kwamba hahusiki na tukio hilo.Na Mtanzania
No comments:
Post a Comment