Baadhi ya
Wawakilishi wa Serikali wakiwa katika kikao cha Kujadili Mapendekezo ya
Vyama vya Siasa juu ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba
yaliyowasilishwa Serikalini tarehe 21 Oktoba 2013, (kutoka kushoto),
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Bi. Angela Kairuki, Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Mhe. Jaji Frederick Werema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge ), Mhe. William Lukuvi (Mb), kikao
hicho kimefanyika leo Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu
Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya
Wawakilishi wa vyama vyenye wawakilishi Bungeni wakiwa katika kikao cha
Kujadili Mapendekezo ya Vyama vya Siasa juu ya Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya katiba yaliyowasilishwa Serikalini tarehe 21 Oktoba 2013,
kikao hicho kimefanyika leo Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya
Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam. (HD)
Serikali
imekutana na Kituo cha Demokrasia nchini ambacho wanachama wake ni vyama
vyenye wawakilishi Bungeni ili Kujadili Mapendekezo ya Vyama vya Siasa
juu ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba ambayo vyama hivyo
viliyawasilisha Serikalini tarehe 21 Oktoba 2013.
Akiongea wakati wa kikao hicho leo Katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi
ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge ), Mhe. William Lukuvi (Mb) alifafanua kuwa
lengo la kikao hicho ni kujadili na kuchambua Mapendekezo ya Vyama vya
Siasa juu ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba ambayo
waliombwa wayawasilishe rasmi.
"Kikao hiki kinafanyika kufuatia kikao alichofanya Mhe. Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe
15 Oktoba Ikulu Jijini Dar es Salaam na Viongozi wa Vyama vyenye
wawakilishi Bungeni na kuwaomba wawasilishe rasmi maoni yao Serikalini
na sasa kamati ya kitaalam ya Serikali tumekutana nao kujadili na
kuchambua Mapendekezo yao" alisema Lukuvi.
Vyama vya Siasa vilivyo shiriki katika kikao hicho ni; CCM, CHADEMA,
CUF, NCCR Mageuzi, UDP na TLP, kwa upande wa Serikali iliwakilishwa na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali , Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), Waziri wa Sheria na Katiba, Naibu Waziri wa
Sheria na Katiba, Msaidizi wa Sheria wa Rais, Msaidizi wa Sheria wa
Waziri Mkuu na Mkurugenzi wa Idara ya Siasa na Bunge Ofisi ya Waziri
Mkuu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment