
Wapigaji wanazidi kuiteka nchi, uthubutu wa vitendo vya uporaji kwa njia
za udanganyifu umeshika kasi na sasa hivi umepiga hodi kwa mke wa
waziri wa zamani.
Ikupa Mwakanjuki, mke wa waziri wa zamani wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, marehemu Brigedia Adam Mwakanjuki,
ametapeliwa shilingi milioni 280.
Waliomtapeli Ikupa ni vijana wanne
ambao inadaiwa ni matapeli wazoefu jijini Dar es Salaam na kwenye baadhi
ya mikoa ya Tanzania, wakitumia ‘triki’ ya uganga wa kienyeji.
Vijana
hao wakijifanya waganga wa kienyeji, walimfuata Ikupa na kumwambia
kwamba wangeweza kumfanya atajirike zaidi kwa njia za mizimu.
Watuhumiwa
wote wanne wa utapeli huo wameshakamatwa lakini gazeti hili limepata
majina ya wawili, wa kwanza akifahamika zaidi kwa jina la Silver na
mwingine ni Mwang’ombe ambaye picha yake inaonekana ukurasa wa kwanza.
Chanzo
chetu kilisema kuwa baada ya mwanamke huyo kupewa maneno ya ulaghai,
aliingilika lakini akawa hana fedha ambazo ‘waganga’ hao walizihitaji.
“Mama
aliposema hana fedha, wale matapeli walimwambia anazo mali ambazo
anaweza kuuza na kupata kiasi cha fedha kinachohitajika,” kilisema
chanzo chetu na kuongeza:
“Mama alisema analo shamba, wakamshawishi
auze. Mama naye sijui aliwekewa nini, akawa anafanya kila kitu kutokana
na maelekezo ya wale matapeli.
“Kweli aliuza shamba lakini fedha zote
alikabidhi kwa wale matapeli. Siku zikapita, haoni mabadiliko yoyote,
ghafla akamuona Mwang’ombe anaendesha gari la kifahari aina ya Toyota
Land Cruiser Prado.
“Hapo ndiyo akashtuka, Mwang’ombe bila woga,
akarudi tena kwa mama akamwambia zinahitajika fedha nyingine kwa ajili
ya sadaka kwa yatima.
“Akiwa na wenzake, wakamshawishi auze shamba
lingine zipatikane japo shilingi milioni 100 ili maisha yaanze
kubadilika kwa kasi. Hapo ndipo akatushirikisha ndugu, tukagundua huo ni
utapeli. Tukaamua kulifikisha hili suala kwenye vyombo vya sheria.”
Habari
zaidi zinasema kuwa Ikupa kwa ushawishi wa ndugu zake, alifikisha
malalamiko yake mpaka makao makuu ya jeshi la polisi na inadaiwa kuwa
IGP Said Mwema aliagiza ma-RPC wote kufanya juu chini na kuwaweka
nguvuni watuhumiwa.
“Hii ishu ni ya juu, sisi tumetumwa tuwakamate,
tukishafanikiwa tutawakabidhi watuhumiwa kwa maofisa upelelezi makao
makuu,” mmoja wa maofisa wa jeshi la polisi Kinondoni, alilinong’oneza
gazeti hili.
Septemba 18, mwaka huu, saa 8 usiku, Mwang’ombe bila
kujua kama yupo mtegoni, alipaki Prado lake lenye namba za usajili T940
CLX, Corner Bar, Sinza Afrika Sana, Dar es Salaam.
Alipopaki hapo,
alichagua kiti ili apate ‘kuzila bata zake’ lakini eneo hilo, alikuwepo
kaka mdogo wa Ikupa ambaye alitoa taarifa polisi na mara moja, gari lake
likazingirwa kabla ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kufikishwa Kituo cha
Polisi Kijitonyama, Mabatini.
Uwazi lilikuwepo wakati Mwang’ombe
anakamatwa Corner Bar na lilipofuatilia, liligundua kwamba mtuhumiwa
huyo alimtaja Silver kwamba naye ni mhusika.
Oparesheni ikitekelezwa
na maofisa upelelezi makao makuu, ilifanikisha kukamatwa kwa Silver eneo
la Kimara Baruti, usiku huohuo na siku iliyofuata, watuhumiwa wengine
wawili walitiwa nguvuni kisha shauri likarejeshwa Oysterbay kwa
utekelezaji wa mkondo wa kisheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, ACP Camillius Wambura, alilithibitishia gazeti hili kwamba
tukio hilo lipo mezani kwake.
“Tupo kwenye uchunguzi, kuna vitu
tunakamilisha halafu baadaye tutafanya mawasiliano na ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili kwenda mahakamani,” alisema
Wambura.
Ikupa alipopigiwa simu, alipokea mtu wake wa karibu ambaye alisema: “Kama mama atataka kuzungumza na wewe atakupigia.”
Baada ya hapo hakupokea tena simu.
Utapeli
kwa njia za uganga, mitandao ya simu, katika mashine za fedha (ATM) na
kadhalika, umekuwa ukishika kasi nchini ingawa jeshi la polisi limekuwa
likijipambanua kwamba linashughulikia kwa nguvu kubwa.CHANZO BONGOCLANTZ