Mahakama nchini Kenya imemtoza
faini ya shilingi milioni 20 au dola laki mbili na thelathini raia mmoja
mchina kwa kuhusika na biashara haramu ya pembe za ndovu.
Adhabu hii inatokana na sheria kali za kudhibiti uwindaji wa wanyama pori.Ikiwa atashindwa kulipa faini hiyo huenda akafungwa miaka saba gerezani.
Kenya iliharamisha biashara ya pembe za Ndovu mwaka 1989, lakini kumekuwa na ongezeko la biashara hiyo haramu katika miaka ya hivi karibuni.
Kuna hitaji kubwa la pembe hizo barani Asia kwa matumizi ya mapambo huku wahifadhi wa mazingira wakishuku kuwa pembe za Vifaru hutumiwa kama dawa Mashariki mwa Bara Asia.
Nchini Kenya kilo moja ya Pembe za Ndovu, inaweza kukugharimu kati ya shilingi 12,000-18,000.
Uwindaji haramu umetajwa kama bishara haramu ya kimataifa ambapo wawindaji hasa huwawinda ndovu na vifaru kwa wingi. Ni hapo jana tu ambapo kifaru mmoja aliyetambulika kwa jina Josephina, aliuawa katika mbuga ya wanyama ya Nairobi.
Kwa muda wa wiki moja nchini Kenya, kimeripotiwa matukio manne ya uwindaji haramu katika mbuga tofauti tofauti.
Mkuu wa shirika la kulinda wanyama pori nchini Kenya, bwana William Kipsang, anasema kuwa tatizo la uwindaji linachangiwa na maswala ambayo hawawezi kudhibiti kama shirika.
''Serikali ya Kenya imetumia mamilioni ya fedha kuhifadhi wanyama pori , lakini nchini Kenya na kwingineko barani Afrika raia wengi wangependa kuona usalama wa binadamu ukishughulikiwa kwanza badala ya wanyama pori. Vile vile watu wengi huishi katika miji iliyo mbali na misitu na wanyama hao,'' alisema Kipsang
Mashirika ya kulinda wanyama wanasema ikiwa tatizo la uwindaji haramu halitatatuliwa, basi kwa muda wa miaka ishirini, ndovu na vifaru barani Afrika hawatokuwepo tena.
Asilimia kumi ya uchumi wa Kenya hutegemea utalii, ikiwa Kenya itapoteza Ndovu na vifaru wake, basi sekta ya utalii itaathirika pakubwa.
No comments:
Post a Comment