Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bado ina upungufu ambao utaathiri
utendaji wa Bunge Maalumu, ambalo huenda likaanza Februari 11 mwaka
huu, mjini Dodoma.
Sheria hiyo Namba 8 ya 2011, imeishafanyiwa
marekebisho mara mbili yakiwamo ya Februari 2012 na Novemba 2013, lakini
mabadiliko hayo yameacha kasoro ambazo zinapaswa zifanyiwe tena kazi,
kupitia Bunge.
Kasoro zipo katika Kifungu cha 22 kinachohusu
uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum, pamoja na kifungu cha 24
kinachozungumzia Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo wanavyoanza
kutekeleza wajibu wao.
Kupitia Sheria ya Marekebisho (Na:2) ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya 2013, Bunge katika mkutano wa 12, liliwapa
mamlaka Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, ‘kufanya
maandalizi muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge
Maalumu’.
Watendaji hao kwa mujibu wa sheria ndio
watakaoteuliwa kuwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu baada ya
Rais kutangaza kuitishwa kwa Bunge hilo, lakini kiapo chao kitasubiri
hadi pale watakapochaguliwa Mwenyekiti na Makamu wa Bunge hilo.
Sheria husika inaweka sharti kwamba ikiwa
Mwenyekiti atatoka upande mmoja wa Muungano basi Katibu atoke upande
mwingine na kinyume chake. Hivyo lazima wasubiri uchaguzi huo ili wajue
ni nani Katibu na Naibu Katibu.
Kifungu cha 24 (2) kinasema: “Katibu na Naibu
Katibu wa Bunge Maalumu, watashika nyadhifa zao kwa misingi kwamba,
endapo Mwenyekiti atachaguliwa kutoka upande mmoja wa Jamhuri ya
Muungano basi Katibu wa Bunge Maalumu atatoka upande wa pili wa Jamhuri
ya Muungano”.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tayari
baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Bunge na ile ya Baraza la
Wawakilishi (BLW) wameanza maandalizi ya awali katika moja ya hoteli za
jijini Dar es Salaam.
Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah mbali na
kukiri kuanza kwa maandalizi hayo, hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani
suala hilo kwa maelezo kuwa lazima ashirikiane na Katibu wa Baraza la
Wawakilishi.
Hata hivyo, kutokana na mkanganyiko mkubwa uliopo
katika Sheria hiyo, ni dhahiri watendaji hao watapata wakati mgumu
katika kuanza kutekeleza majukumu, hasa katika kuteua wajumbe wa
sekretarieti ya Bunge hilo.
Uteuzi wa wajumbe hao kwa mujibu wa kifungu cha 24
(4) unapaswa kufanywa na Katibu kwa kushauriana na Naibu wake, nafasi
ambazo hazitakuwapo hadi pale Mwenyekiti na Makamu wake
watakapochaguliwa
.
Fursa ya marekebisho
Hivi sasa hakuna fursa kwa Bunge la Muungano kufanya marekesho
katika sheria hiyo ili kuondoa mkanganyiko uliopo, kwani kikao chake
ambacho kilipaswa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu hadi mwanzoni mwa
Februari, kilifanyika Desemba mwaka jana, ili kutoa fursa kwa Bunge
Maalumu.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Angela Kairuki alisema jana kuwa ikiwa kuna kasoro zozote
zitakazojitokeza, wataalamu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa
Baraza la Wawakilishi watazifanyia kazi.
“Kuwapo kwa upungufu katika sheria zinazotungwa
huwa ni jambo la kawaida, lakini pili katika sheria huwezi kuandika kila
kitu na ndiyo maana katika mabadiliko yaliyofanyika Katibu wa Bunge na
mwenzake wa Baraza la Wawakilishi walipewa wajibu wa kisheria kufanya
maandalizi,” alisema Kairuki na kuongeza:
“Na tulifanya hivyo makusudi kwani tunata uzoefu
uliopo katika vyombo hivi utumike katika kuendesha Bunge la Katiba, mimi
ninawaamini wataalamu wetu kwa hiyo hakuna kitakachoharibika.”
Vifungu vinavyokanganya
Kifungu cha 22 kimeweka masharti kwamba baada ya
kuitishwa kwa Bunge hilo, Katibu wa Bunge la Muungano na Katibu wa
Baraza la Wawakilishi, watasimamia mchakato wa kumchagua Mwenyekiti wa
muda wa Bunge Maalumu.
Kadhalika, kifungu cha 24 (5) cha Sheria hiyo
kinasema: “ Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum, kabla ya kushika
madaraka yao wataapa au kula yamini mbele ya Rais”. Kwa maana hiyo,
watendaji hao watasimamia uchaguzi wa mwenyekiti wa muda pasipokuwa na
nguvu ya kisheria kwani watakuwa hawajala kiapo kutokana na kutofahamu
nafasi zao; ni yupi Katibu na Naibu Katibu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa muda ambaye
anachaguliwa kwa mujibu wa Kifungu cha 22 (a) na (b), ndiye
atakayesimamia uandaaji na upitishwaji wa Kanuni za Bunge Maalum na
kuendesha uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo.
Lakini ni dhahiri kwamba Mwenyekiti wa muda
atachaguliwa bila kuwapo kwa kanuni, huku kukiwa hakuna utaratibu wowote
wa kisheria anaoelekeza jinsi atakavyopatikana.
Kadhalika kifungu cha 26 (1) cha Sheria hiyo
kinataka shughuli zote za Bunge Maalum ziendeshwe kwa kufuata Kanuni
husika na pia kifungu cha 24 (3) kinawataka watendaji watatekeleza
majukumu yao kwa mujibu wa Kanuni hivyo uchaguzi wa Mwenyekiti wa muda
na usimamizi wake lazima vizingatie kanuni jambo ambalo haliwezekani
kwani zitakuwa hazijapitishwa.
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment