Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza
Mhe. Nick Clegg walipoikutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya
Sheraton Davos, Uswisi.
Serikali
ya Uingereza imesema kuwa inatafakari ombi la Tanzania la mabehewa na
injini za treni ambayo nchi hiyo haizitumii tena lakini bado ni nzima
kwa ajili ya kusaidia kuimarisha usafiri wa reli katika Tanzania na
hasa wa Jiji la Dar Es Salaam.
Ahadi
hiyo ya Uingereza ilitolewa na Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza Mheshimiwa
Nick (Nicholas William Peter) Clegg wakati wa mazungumzo yake na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
kwenye hoteli ya Sheraton, Davos, Uswisi, ambako viongozi hao wawili
walikuwa wanahudhuria Mkutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani (WEF) mwaka
huu.
Katika
mazungumzo yao katikati ya wiki hii, Rais Kikwete alizungumzia hatua za
Serikali ya Tanzania za kuimarisha usafiri hasa ule wa reli mjini Dar Es
Salaam na ile ya kwenda Bara.
Katika
mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika Mheshimiwa Christopher Chiza na Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa
Harrison G. Mwakyembe, Rais alimwomba Mheshimiwa Clegg kuangalia
uwezekano wa nchi hiyo kutoa mabehewa na injini ambazo hazitumiki tena
katika Uingereza ambako Rais alisema kuwa bila shaka bado zinafaa kwa
Tanzania.
Akielezea
hali ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli nchini, Waziri
Mwakyembe alisema kuwa kutokana na uchakavu wa reli na ukosefu wa injini
na mabehewa ya kutosha ni kiasi cha tani 300,000 tu za mizigo
zinazosafirishwa kwa reli kati ya mizigo tani milioni 13.7 ambayo
inasafirishwa nchini kila mwaka. Alisema kuwa kiasi kilichobakia
kinasafirishwa kwa barabara.
“Mheshimiwa
unaweza uzito wa ninayoyasema kwa sababu tunajenga barabara nyingi
nchini, kila kona, lakini usafirishaji wa namna hii wa mizigo kwa
barabara utaharibu kabisa barabara hizo katika muda mfupi,” Rais Kikwete
alimwambia Mheshimiwa Clegg
Katika
mazungumzo hayo, Rais Kikwete aliishukuru Serikali ya Uingereza kwa
kuendelea kuunga mkono maendeleo ya Tanzania kwa kusaidia nyanja za
elimu, afya na maji na pia kuendelea kuwa nchi inayoongoza duniani kwa
makampuni yake kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Rais pia
alimwomba Mheshimiwa Clegg kusaidia kuvutia uwekezaji zaidi kutoka
Uingereza kuja Tanzania kwa kuisemea vizuri Tanzania. “Neno lako moja la
kusifia Tanzania lina nguvu zaidi kuliko hotuba zangu kwa makampuni na
wenye makampuni katika Uingereza.”
Viongozi
hao pia walizungumzia umuhimu wa kukamilisha Mikataba ya Ushirikiano wa
Uchumi ya EPA kati ya nchi za Afrika na nchi za Ulaya. Walikubaliana
kuwa mjadala wa jambo hilo umechukua muda mrefu kupita kiasi na sasa ni
wakati wa kufikia mwisho wa jambo hilo.
Rais
Kikwete alimwambia Naibu Waziri Mkuu huyo kuwa moja ya sharti ambalo
yanayoikwaza Afrika katika kufikia makubaliano ya mikataba hiyo ni lile
la kuzilazimisha nchi za Afrika kufungua masoko yao kwa namna ile ile ya
yatakavyofunguliwa masoko ya nchi za Ulaya.
“Hofu
yetu hasa ni kuhusu jambo hilo. Ni vigumu, kwa mfano, kwa makampuni ya
ujenzi ya Tanzania kushindania tenda moja na kwa masharti yale yale na
makampuni ya Uingereza kwa sababu wakati mwingine unaweza kufungua
uwanja ukawa sawa lakini wachezaji wasiwe na uwezo unaofanana.”
Wakati wa
mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimkaribisha Mheshimiwa Clegg kutembelea
Tanzania, ombi ambalo Naibu Waziri Mkuu alikubali kimsingi akisema kuwa
anatamani sana kuja tena Tanzania kwa sababu miaka 13 iliyopita
aliitembelea Tanzania kwa mapumziko na mkewe baada ya kuwa wamefunga
ndoa.
No comments:
Post a Comment