Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma kamishna msaidizi mwandamizi DAVID
MISIME (SACP) anawashukuru wananchi wa kondoa kwa jinsi walivyotoa
ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kufanikisha kumkamata mwanamke
aliyeiba mtoto mchanga wa siku moja tarehe 20.01.2014 huko katika maeneo
ya Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.
Mtoto huyo wa jinsia ya kiume alizaliwa tarehe 19.01.2014 huko katika
zahanati ya Thawi. Mama yake mzazi SALMA S/O ZUBERI, mpare, mkazi wa
kijiji cha Mwembeni, Kata ya Changaa - Kondoa, alipatwa na matatizo
ambayo yalimlazimu kuhamishiwa katika hospitali ya Wilaya ya Kondoa.
Wakati mama huyo akiwa anapatiwa matibabu na daktari alibidi mkwe wake
aitwaye HADIJA D/O SAID awe anambeba mtoto huyo mchanga. Alitoka naye
nje na ndipo akakutana na AMINA D/O JUMANNE MWASI, 22 Yrs, mkazi wa
Mningani, Kondoa mjini, alianza akuongea na nyanya wa kichanga hicho cha
siku moja baada ya kuzoeana na mwanamke ambaye alijieleza kuwa
amelazwa hapo hospitali kutokana na ujauzito aliomba kumshika au
kumpakata mtoto huyo.
Mama mkwe huyo alitoka kwenda kutafuta chakula ili mgonjwa
atakapomaliza matibabu aweze kula. Baada ya muda alirudi akashangaa
kutokumwona mama ambaye naye alikuwa amejifanya ni mjamzito haonekani,
alijaribu kumtafuta maeneo mbalimbali na kuuliza watu mbalimbali bila
mafanikio ndipo akaamua kutoa taarifa Polisi.
Kwa vile taarifa zilikuwa zimetolewa maenoe mbalimbali wananchi wema
walimtilia mashaka mwanamke aliyeiba mtoto na andipo kwa ushiriano
mkubwa baada ya kumfuatilia kwa karibu sana Polisi wakafanikiwa kumtia
mbaroni tarehe 29.01.2014 wakati alipompeleka motto huyo hospitali ya
Wilaya kwani mtoto alianza kuugua.
Baada ya mahaojiano alikubali kuwa alimuiba mtoto huyo na hata uchunguzi
wa kitaalamu umebaini mwanamke huyo hajajifungua siku za karibuni.
Ninatoa wito kwa wananchi kutokuamini watu wasiwafahamu kwa asilimia
mia, hata kama wanalugha nzuri kiasi gani pia nawatahadharisha wanawake
waliokosa watoto kwa muda mrefu utatuzi wake sio kuiba watoto wa watu
wengine.
DAVID MISIME – SACP
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA


No comments:
Post a Comment