Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, January 16, 2014

VIBAKA WAVAMIA, WAIBA NYUMBANI KWA NYERERE


NYUMBA ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, inayotumiwa na mjane wake, Mama Maria na familia, wiki hii imevamiwa na vibaka usiku na kuvunjwa. Taarifa zilizofikia gazeti hili jana zilibainisha kuwa vibaka hao walipitia upande wa ufukweni usiku wa manane, wakavunja dirisha na kuingia.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, vibaka hao walitoweka na televisheni, ambayo haikutajwa aina wala ukubwa na kompyuta ya mkononi aina ya Toshiba.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema nyumba hiyo ilivamiwa Januari 11 kati ya saa 8 usiku na alfajiri.
Alithibitisha kuwa wezi hao waliingia ndani ya uzio na kuiba televisheni na kompyuta mpakato. Kamanda Wambura alisema kabla ya saa 8 usiku kuna watu walikuwa macho, lakini baada ya muda walikwenda kulala na walipoamka asubuhi wakakuta wameibiwa.
"Ndani ya uzio huo kwa pembeni kuna nyumba anamoishi mjukuu wa Mwalimu Nyerere, na huko ndiko waliingia na kuiba televisheni na hiyo kompyuta baada ya kukata waya wa dirisha," alisema Kamanda Wambura.


Alisema taarifa ya tukio hilo imefunguliwa jalada katika kituo cha Polisi Oysterbay na kupewa namba OB/RB/822/2014.
Kamanda alimtaja mjukuu wa Mwalimu aliyeibiwa kuwa ni Moringe Nyerere (30), ambaye anafanyakazi katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), na anaishi katika nyumba hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Wambura, tayari mtu mmoja amekamatwa akihisiwa kushiriki wizi huo ambaye hakumtaja jina, lakini alisema alipata kufanya kazi katika nyumba hiyo na baadaye kufukuzwa.
"Kuna kijana walimhisi kufanya wizi huo ambaye alikuwa akifanya kazi hapo kwa karibu miaka miwili lakini alifukuzwa kutokana na tabia ya udokozi, siku mbili kabla ya wizi huo alionekana hapo na alipoondoka wizi huo ukafanyika," alisema Kamanda Wambura na kuongeza kuwa kuna mtuhumiwa mwingine anatafutwa.

HABARI LEO

No comments:

Post a Comment