Na
Gideon Mwakanosya -Mbambay
Baadi ya wananchi
wanaoishi katika vijiji vilivyoko kandokando ya ziwa Nyasa katika wilaya ya
Nyasa Mkoa wa Ruvuma wamewalalamikia baadhi ya wananchi wakiwemo wavuvi wa
samaki kwa tabia yao ya kutumia vibaya vyandarua tofauti na makusudio yake ambapo
serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa muda mrefu imekuwa ikigawa vyandarua bure
lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia kuvulia samaki huku wengine
wakitumia kuanikia dagaa kwenye vichanja.
Wakizungumza na NIPASHE,
kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Mbaha na Lundu wananchi hao ambao
waliomba majina yao yafadhiwe walisema kuwa serikali imekuwa ikigawa vyandarua
kwa kila kaya kwa lengo la kupunguza malaria lakini ni jambo la kushangaza
baadhi ya wavuvi na wakazi wengine wamekuwa wakitumia vyandaraua hivyo tofauti
na ilivyokusudiwa.
Walisema kuwa katika
vijiji vingi vilivyoko kandokando ya ziwa Nyasa kumekuwa na tabia hiyo mbaya
ambayo inaweza kuhatarisha maisha kwa wakazi wa maeneo hayo ya kuchukua
vyandarua kwenye majumba na kupeleka ziwani kuvulia samaki huku wengine wakanikia
dagaa wakati wanajua kwamba vyandarua hivyo vimewekwa dawa za viuatilifu.
Wameiomba serikali ya wilaya
hiyo kuona umhimu wa kuwazuia au kuwapiga marufuku kuvulia na kuanikia samaki vyandarua
na badala yake wananchi wahimizwe kuvitumia vyandarua kama ilivyokusudiwa na
serikali na sio vinginevyo.
Hata hivyo mratibu wa
malaria wa mkoa wa Ruvuma, Kibua Amani Kakolwa, alisema kuwa kampeni ya ugawaji
vyandarua sehemu za malazi ilifanyika mwaka 2010 ambapo jumla ya vyandarua
706219 viligawiwa kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma wakti vyandarua 236375 viligawiwa katika wilaya ya Mbinga
kabla kabla wilaya hiyo haijagawanywa.
Kibua alisema kuwa lengo
kuu ni kuwa wananchi wanapaswa kuvitumia kila siku ili waweze kujikinga na mbu
waenezao malaria na uwezo wa vyandarua hivyo ni miaka mitatu hadi mitano kama
vinatunzwa vizuri hivyo watu wanaoamua
kuanikia au kuvulia dagaa wanakwenda tofauti na malengo ya serikali.
Aliongeza kuwa faida ya
vyandarua itaonekana katika kupunguza malaria endapo kila mwananchi atatumia
chandarua chake kwa usahihi na amezishauri mamlaka za halmashauri za wilaya
zitumie sheria ndogo walizo nazo kuhakikisha kuwa wananchi hawatumii vyandarua
kwa shughuli ambazo hazikukusudiwa na serikali.
Kwa upande wake mkuu wa
wilaya ya Nyasa, Ernest Kahindi, aliiambia NIPASHE kuwa ofisi yake ilishapokea
malalamiko hayo na kwamba kwa hivi sasa amewaagiza viongozi wote wa serikali
wakiwemo maafisa watendaji wa vijiji na kata kuwa mwananchi yeyote
atakayepatikana kuainikia dagaa au
kuvulia samaki akamatwe na achukuliwe hatua haraka iwezekanavyo na maafisa wa
idara ya maliasili tayari wameshaanza kufanya msako kijiji hadi kijiji
kandokando ya Ziwa Nyasa ili kuwabaini waharibifu wa vyandarua.
No comments:
Post a Comment