Rais
Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha urafiki wa
dhambi na baadhi ya wachimbaji wakubwa wanaohodhi maeneo makubwa na
badala yake wazingatie sheria ili kutoa haki kwa wachimbaji wadogo.
Akizungumza
katika siku yake ya mwisho kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa Baraka uliopo
wilayani Geita katika Kijiji cha Nyaruyeye juzi, Rais Kikwete alisema
kilio cha wachimbaji wadogo hivi sasa ni maeneo lakini wanaweza kuchimba
sawa na wachimbaji wakubwa hivyo kuitaka wizara hiyo kuzingatia sheria
kwa kuwafutia umiliki wenye maeneo ambayo hawayafanyii kazi.
“Mkiyatwaa
watapiga kelele, acheni wapige kelele lakini timizeni sheria. Masele
(akimwangalia Naibu Waziri Nishati na Madini Stephen Masele) na wenzako
lazima mzingatie sheria. Wanyang’anyeni maeneo haya wapeni wachimbaji
wadogo wachimbe. Acheni kufanya urafiki wa dhambi na hawa,” alisema Rais
Kikwete.
Rais
Kikwete ambaye alieleza kufurahishwa kwake na wachimbaji wadogo kuanza
kuchimba kisasa alisema sheria ya umilikaji wa maeneo ya utafiti na
uchimbaji wa madini inaelekeza kuwa iwapo mwombaji akija kuomba tena
(renewal) leseni ya eneo alilopewa anapaswa kulipunguza kwa asilimia 50
ili wapewe wengine na vivyohivyo anapokuja kwa mara ya pili, pia
anapaswa kupunguziwa eneo lake kwa asilimia 50.
“Pamoja
na kwamba sheria ipo wazi, ukiwauliza wizara kwa nini hawafanyi hivyo,
hawana maelezo wapo kimya, sijui wanaingia kigugumizi gani kutimiza
sheria hii. Wanaposhindwa kufanya haya ni hasara kwa taifa maana haya
madini hayachimbwi, wangezingatia sheria hii na kuchukua maeneo haya
wangewapa wengine wakachimba leo tusingekuwa na kelele za wachimbaji
wadogo,” alisema. Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana
thamani yoyote mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu
waliopewa leseni watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao,
watakwamisha ajira na maendeleo kwa nchi.
Aidha,
aliitaka wizara hiyo kuwa makini wakati wa kutimiza matakwa ya sheria
hiyo ya umiliki wa maeneo ya uchimbaji, akitahadharisha kuwa wamiliki
wengine wanaweza kubadili majina pindi watakaponyang’anywa maeneo yao.
“Wana
tabia ya kubadili majina, mkimnyang’anya atakuja upya. Kama alikuwa
anaitwa Kikwete & Sons sasa atakuja tena anajiita SK lakini ndiye
huyohuyo, tazameni sana. Najua, mnayajua mengi maana na ninyi ni wabia
wao lakini ninachotaka ni kuzingatia na kusimamia sheria,” alisema.
Akizungumzia
Mgodi wa Mzawa alioutembelea, Rais Kikwete alisema amejionea jambo
kubwa na la kushangaza kiasi cha kusema kwamba iwapo angeishia
kusimuliwa mambo hayo na watu bila ya kufika, asingeamini kama
Watanzania wanaweza kuendesha migodi kama huo.
Alisema
Serikali inathamini mchango wao na kuwataka kujiandikisha Tume ya
Uwekezaji ili nao waweze kuomba msamaha wa mafuta na zana mbalimbali
kama ilivyo kwa wawekezaji wakubwa wa nje.
Awali,
Masele alimwomba Rais kuangalia uwezekano wa kuwapatia wachimbaji
wadogo msamaha wa kodi akisema vifaa wanavyotumia havina tofauti na vile
vya wachimbaji wakubwa.
No comments:
Post a Comment