Na Aron Msigwa –MAELEZO.
Watanzania
wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kupima
afya na kuepuka tabia hatarishi zinazochangia uwezekano wa kupata
ugonjwa wa kisukari.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii Dkt. Hussein Mwinyi wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu Siku ya
Ugonjwa wa Kisukari Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 14.
Amesema
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine inaadhimisha siku hiyo kwa Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa
kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na
madhra mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huo.
Amesema
maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani 2013 yataongozwa na kauli mbiu
isemayo “Linda Maisha yajayo dhidi ya Ugonjwa kisukari” inayolenga
kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali yanayotokana na ugonjwa wa
kisukari katika jamii.
Ameeleza
kuwa athari za ugonjwa wa kisukari katika mwili wa binadamu hutokea
wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida
kwa muda mrefu na kuongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mwaka 2007
kulikua na wagonjwa milioni 246 duniani huku mwaka 2012 kukiwa na
wagonjwa milioni 371 ambapo nusu ya idadi ya wagonjwa hao walikua
hawajaanza kupata matibabu.
Kuhusu
dalili za ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni rahisi kuzitambua
na huambatana na mgonjwa kuwa na kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara,
kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu na
kuongeza kuwa athari za ugonjwa huo ni kubwa kutokana na ugonjwa huo
kuharibu mishipa ya damu na fahamu, macho, figo, kusababisha upofu, moyo
na figo kushindwa kufanya kazi na miguu kufa nganzi na kuwa na vidonda.
Dkt.
Mwinyi ameeleza kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wote duniani wanaishi
katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania na kuongeza kuwa utafiti
uliofanyika mwaka 2012 nchini Tanzania kwa kuzihusisha wilaya 50
unaonyesha kuwa asilimia 9.1 ya watanzania wenye umri wa miaka 25 na
kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.
“Ni
jambo lililo wazi kuwa lazima tubadili tabia hasa tabia hatarishi
zinazochangia ugonjwa wa kisukari zikiwemo unywaji wa pombe kupita
kiasi, ulaji usiofaa, ulaji usiofaa na tabia ya kupuuza kufanya
mazoezi”, sasa Tanzania katika nchi 10 za Afrika zinazoongoza kwa
kisukari barani Afrika inashika nafasi ya 8” Amesema Dkt. Mwinyi.
Kuhusu
sababu zinazochangia ugonjwa huo Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na
tabia ya ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi , mafuta na
sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi , uvutaji
wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku pamoja, kula vyakula vyenye
mafuta mengi hasa yatokanayo na wanyama, sukari nyingi,kula chakula
kupita kiasi, kukoboa nafaka, kutokula mbogamboga na matunda na unywaji
wa pombe kupita kiasi.
Ameeleza
kuwa jamii inapaswa kuepuka mambo yanayochangia chakula kilicholiwa
kutotumika vizuri ikiwemo tabia ya kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi
huku akisisitiza kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi huharibu maini na
kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe Zaidi bila kula
chakula.
“
Natoa ushauri hasa kwa watumishi kuepuka kuketi ofisini, darasani au
kuangalia runinga kwa muda mrefu na hata kutumia lifti kwenda ghorofani
badala ya ngazi na matumizi ya magari katika umbali mfupi unaoweza
kufikika kwa kutembea tu”
Dkt.
Mwinyi ameleza kuwa serikali imejipanga kukabiliana na changamoto
mbalimbali zinazotokana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa utekelezaji wa
Sera ya Afya ya mwaka 2007 unaendelea kwa kuhakikisha kuwa utoaji wa
hudunma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari unafanyika kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Ameeleza
kuwa serikali kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari
kuanzia mwaka 1983 ilitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa wote wa
kisukari kutochangia gharama za matibabu pia kuhakikisha kuwa dawa
muhimu zinapatikana katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini.
Kwa
upande wake Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Donan Mmbando amewataka vijana
kote nchini ambao ni kundi kubwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi
mara kwa mara na kuepuka maisha ya anasa ambayo huwaweka katika hatari
kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari.
Amesema
mapambano ya ugonjwa wa kisukari yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi
hasa kuzingatia kanuni za Afya na kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara
mara.
No comments:
Post a Comment