UPO msemo uliotawala vichwa vya watu tangu dahari kwamba
wanawake ni tabaka la kukaa nyumbani na kufanya kazi za ndani. Wao jukumu lao
ni kumfurahisha mume na lingine ni kuwaandaa watoto kwa ajili ya kwenda shule
na kufuatilia nyenendo zao darasani.
 |
Miss Tanzania aliyechukua taji hilo mwaka 2001, Happiness
Magesse ndiye aliyefanikiwa zaidi kimataifa kuliko wote, japo wapo wengine
wanaojitahidi. Hivi sasa Happiness ‘Millen’ ni mwanamitindo wa kimataifa.
|
Happiness Magesse.
Ilivyozoeleka ni kwamba wanawake ni goigoi. Utaona bungeni
kuna wabunge wa viti maalum ambavyo wengi hutafsiri kuwa ni vya upendeleo. Kwa
maana kwamba uwezo wao kushindana kwenye majimbo na kushinda ni mdogo ndiyo
maana wanapewa hivyo maalum kwao.
Katika mitihani, kuna unafuu wa alama za ufaulu kwa
wanafunzi wa kike. Yaani wanaonekana hawana uwezo wa kushindana na wavulana.
Vijijini, wanawake wamekuwa wakitumika kama nyenzo ya kilimo, yaani mama
akalime ndiyo alishe familia, baba akacheze bao au kunywa pombe.
Miaka inakwenda, wapo wanawake wengi ambao wameweza kudhihirisha
kwamba inawezekana kwa jinsi ya kike kuanzisha kazi na kufanikiwa. Aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ni mfano wenye
nguvu kwa wanawake kufanikiwa.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mchungaji Getrude Rwakatare na
wengineo, ni kichocheo kinachotoa uthibitisho kuwa wanawake wanaweza. Ni suala
la kuwaamini na kuwapa nafasi, kwa hakika wanaweza kufanya mambo makubwa mno.
Ukiachana na hao, ipo orodha ya wanawake vijana 10 ambao
wanastahili pongezi. Wamepambana katika maeneo yao kiasi cha kupata mafanikio
ambayo yameonesha njia. Inabidi tuwatambue na kuthamini jitihada zao kwa maana
wameendelea kuthibitisha ndivyo sivyo kwa wale waliokuwa wanaamini kuwa
wanawake si lolote kwenye utafutaji.
FLAVIANA MATATA
Mwaka 2007 alipokwenda kushiriki mashindano ya dunia ya Miss
Universe na kushika nafasi ya sita, wengi walidhani huo ndiyo mwisho wake.
Ilionekana hivyo kwa sababu warembo wengi wameshiriki mashindano ya dunia na
baada ya kurudi nchini, hawakusikika tena.